Baha na mpenzi wake Georgina Njenga wavunja kimya kuhusu kuachana

Kumekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya mahusiano ya wazazi hao vijana.

Muhtasari

•Tyler Mbaya na mpenzi wake Georgina Njenga wamethibitisha kwamba bado wako mahusiano yao bado yapo imara.

•Wakenya mitandaoni wamekuwa wakiwazungumzia wawili hao, huku baadhi yao wakidai kuwa hawako pamoja tena.

Muigizaji Tyler Mbaya na mpenzi wake Georgina Njenga
Image: INSTAGRAM// TYLER MBAYA

Muigizaji Tyler Mbaya na mpenzi wake Georgina Njenga wamethibitisha kwamba bado wako mahusiano yao bado yapo imara.

Siku ya Jumatano, Tyler ambaye anafahamika zaidi kama Baha kutokana na kipindi maarufu cha Machachari kwenye runinga ya Citizen TV alichapisha video iliyomuonyesha akicheza na mzazi huyo mwenzake.

Katika video hiyo ambayo ilichapishwa kwenye mtandao wa Tiktok, wazazi hao wa binti mmoja walionekana wakicheza densi ya mwendo pole pamoja huku wakisikiliza wimbo mpya wa Iyanii 'Cheat on Me'. 

Tyler pia aliambatisha video hiyo yake na mpenziwe na emoji ya moyo (❤️)  kuashiria mahaba mazito kati yao.

Bi Georgina pia alichapisha video hiyo nzuri kwenye akaunti yake, ishara wazi kwamba uhusiano kati yao bado ni mzuri.

Katika kipindi cha wiki kadhaa ambazo zimezopita, kumekuwa na maswali chungu nzima juu ya hali ya mahusiano ya wazazi hao vijana.

Wakenya mitandaoni wamekuwa wakiwazungumzia wawili hao, huku baadhi yao wakidai kuwa hawako pamoja tena.

Mwaka uliopita, wenzi hao walikabiliwa na nyakati za majaribu baada ya video chafu zilizodaiwa kuwa za Georgina kusambazwa.

Baadaye hata hivyo Baha alimhakikishia mpenzi huyo wake kuhusu mahaba yake mazito kwake licha ya video hizo kuvuma.Aliweka wazi kuwa tukio hilo halikutikisa mahusiano yao hata na kuthibitisha kuwa bado wako pamoja.

"Mapenzi yapo, mapenzi hayawezi tingishwa na sio hoja kwa hili," alisema katika mahojiano na kituo moja cha redio cha hapa nchini.

Wakati huo, Bi Georgina alidai kwamba mpenzi wake wa zamani ndiye aliyehusika katika uvujishaji wa video hizo chafu.

Wakati akimjibu mwanablogu wa humu nchini, alidokeza aliyekuwa mpenziwe hakufurahishwa na uhusiano wake na Tyler.

"Ilitokea nikiwa na miaka 17 na mtu niliyempenda," alisema Georgina.

Aliongeza; "Alianza kunitisha mara tu baada ya kufichua uhusiano wangu na Tyler mwaka wa 2020."

Georgina na Tyler wamekuwa pamoja kwa miaka kadhaa na walibarikiwa na binti mmoja, Astra Nyambura mwaka jana.