"Kama si mimi, usingefaulu” Diana Marua awatupia vijembe wapenzi wa zamani wa Bahati

Bahati alibainisha kuwa alimsaidia mkewe kuacha maisha ya anasa na kuanzisha familia

Muhtasari

•Diana  alimweleza Bahati kwamba hangekuwa amefanikiwa ikiwa hangekuja katika maisha yake zaidi ya nusu muongo uliopita.

•Bahati hata hivyo alimwomba mkewe aache kuchukua sifa ya Mungu akitaja kuwa mafanikio yake yametokana na neema yake.

Diana Marua na mumewe Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu na rapa maarufu Diana Marua amechukua sifa zote kwa mafanikio makubwa ya mpenzi wake Kelvin Kioko almaarufu Bahati.

Wakati wakishiriki mazungumzo ya wazi nyumbani kwao, Diana  alimweleza mwanamuziki huyo kwamba hangekuwa katika nafasi ambayo yuko kwa sasa ikiwa hangekuja katika maisha yake zaidi ya nusu muongo uliopita.

"Naweza kukuambia kitu? Unajua isingekuwa mimi, leo usingekuwa na nyumba hii. Isingekuwa mimi, usingepata watoto hawa. Isingekuwa mimi, usingekuwa na magari manne yameegeshwa hapa," Diana alimkumbusha Bahati.

Mama huyo wa watoto watatu alimweleza mwimbaji huyo kwamba usaidizi ambao amempa ni dhibitisho la kweli la mapenzi.

Bahati hata hivyo alimwomba mkewe aache kuchukua sifa ya Mungu akitaja kuwa mafanikio yake yametokana na neema yake.

"Utukufu wa Mungu u ndani yangu, nina Mungu ndani yangu, kazi za Mungu zipo ndani yangu. Kimsingi nina Mungu ndani yangu. Nikisema nisingekuwa mimi, ni kutoka ndani yangu. Kwa hiyo, usingekuwepo popote bila mimi Bahati. Ungekuwa unateseka. Utukufu wa Mungu ndio umeniangazia," Diana alijibu.

Rapa huyo alionekana kuwatupia vijembe wapenzi wa zamani wa mwimbaji huyo huku alidokeza kwamba wanawake ambao Bahati alikuwa akichagua siku za awali hawangemletea mafanikio makubwa aliyo nayo.

Bahati kwa upande wake alibainisha kuwa alimsaidia mwanavlogu huyo kuacha maisha ya anasa na kuanzisha familia.

"Kama isingekuwa mimi, zile klabu zinafungwa zingekuwa zinafungwa ukiwa ndani. Ungekuwa huko tu unaserereka unauliza utapata watoto lini alafu unajibu 'bado niko mdogo'" Bahati alimwambia mkewe.

Aliongeza,"Mimi ndio nilikwambia haya mambo ya kuwa mdogo."

Wakati wa mazungumzo hayo, Diana alifichua hakuwa tayari kwa ndoa  wakati alipokutana na mume wake  Bahati. Mama huyo wa watoto watatu alidai mwimbaji huyo alimnasa kwenye ndoa yao ya sasa.

Alisema kuwa Bahati alimpa ujauzito katika mwezi wa saba wa uchumba wao na kuwapelekea kwenye ndoa.

"Ulininasa katika mwezi wa saba. Ulininasa. Lakini mpenzi ulikuwa unanipenda. Ulikuwa unakuja na hiyo Mercedes ya bluu kutoka Ruaka hadi Syokimau. Sijui mbona ulikuwa unakuja kwangu saa sita usiku," Diana alisimulia.

Wakati huo, Bahati alifichua kuwa yeye ndiye aliyemfanya mkewe kuondoa chombo alichokuwa nacho mwilini kuzuia mimba.

"Ulikuwa unadanganya wapenzi wako wa zamani eti huna coil. Huenda pengine walidhani wao ni gumba," alisema.

Huku akijitetea, Diana Marua alibainisha kuwa alichukua hatua ya kufunga uzazi kwa kuwa kuna wanaume ambao walikuwa wanampatia zawadi nononono wakiomba kupata mtoto naye, jambo ambalo hakutaka.

"Hawakujua niko na coil ili wajaribu waone hakuna kinachofanyika ili waende," alisema.