Diana Marua afunguka jinsi Bahati alimtoa kutoka maisha ya anasa hadi kwenye ndoa

Bahati alisema yeye ndiye aliyemfanya mkewe kuondoa chombo cha kuzuia mimba alichokuwa nacho.

Muhtasari

•Akizungumza kwenye chaneli yake ya YouTube, mama huyo wa watoto watatu alidai mwimbaji huyo alimnasa kwenye ndoa yao ya sasa.

•Diana alifichua alichukua hatua ya kufunga uzazi kwa kuwa kuna wanaume ambao walikuwa wanampatia zawadi nononono wakiomba kupata mtoto naye, jambo ambalo hakutaka.

Diana Marua na mumewe Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua amefichua kwamba hakuwa tayari kwa ndoa wakati alipokutana na mume wake Kelvin Kioko almaarufu Bahati.

Akizungumza kwenye chaneli yake ya YouTube, mama huyo wa watoto watatu alidai mwimbaji huyo alimnasa kwenye ndoa yao ya sasa.

Wanandoa hao walikuwa wanashiriki mazungumzo ya wazi kuhusu maisha yao ya siku za nyuma wakati Diana Marua alipofichua kuwa Bahati alimpa ujauzito katika mwezi wa saba wa uchumba wao na kuwapelekea kwenye ndoa.

"Ulininasa katika mwezi wa saba. Ulininasa. Lakini mpenzi ulikuwa unanipenda. Ulikuwa unakuja na hiyo Mercedes ya bluu kutoka Ruaka hadi Syokimau. Sijui mbona ulikuwa unakuja kwangu saa sita usiku," Diana alisimulia.

Wakati huo, Bahati alifichua kuwa yeye ndiye aliyemfanya mkewe kuondoa chombo alichokuwa nacho mwilini kuzuia mimba.

"Ulikuwa unadanganya wapenzi wako wa zamani eti huna coil. Huenda pengine walidhani wao ni gumba," alisema.

Huku akijitetea, Diana Marua alibainisha kuwa alichukua hatua ya kufunga uzazi kwa kuwa kuna wanaume ambao walikuwa wanampatia zawadi nononono wakiomba kupata mtoto naye, jambo ambalo hakutaka.

"Hawakujua niko na coil ili wajaribu waone hakuna kinachofanyika ili waende," alisema.

Mama huyo wa watoto watatu alifichua kwamba siku aliyokutana na mwimbaji huyo alikuwa amevunjwa moyo asubuhi yake.

Alifichua kwamba usiku moja walifanya mapenzi bila kinga ambapo mwimbaji huyo alienda nyumbani akiwa na uhakika kwamba amemtunga mimba kwani hakujua kwamba alikuwa amefunga uzazi.

"Bahati alifanya ile kitu. Baada ya kufanya hivyo, alinipigia siku tatu baadaye. (Ndio dawa ya kuzuiwa ifanye kazi, huwa inachukua siku tatu. Ikipita siku tatu wewe jua uwezekano wako kupata mimba ni 90%). Bahati alipiga siku tatu  baadaye wakati nikiendesha gari akanijulia hali," Diana alisimulia.

Mwanablogu huyo alifichua kwamba Bahati alihangaika sana kutafuta maneno ya kumwambia kuwa huenda ni mjamzito.

Alisema wakati huo alidhani mwimbaji huyo ni kama wanaume wengine ambao wangefikiria kumpa ujauzito bila kujali.

"Nilijiuliza eti sasa huyu kijana anafikiria nitaenda kwake kulalamika eti alinitunga mimba ati kwa sababu yeye ni celeb. Nilijiambia mimi siwezi. Hiyo ndiyo ilinipata kwenye mawazo yangu," Diana alisema.

Diana alikiri kuwa alidhani tukio hilo lingekuwa mwisho wa mahusiano yao.