Kwa mara ya kwanza Alikiba na Diamond watakuwa na shoo siku moja nchini Kenya

Wasanii hao ambao wamekuwa wakihasimiana kwa muda mrefu watakutaka kwenye udongo wa Kenya Oktoba 28.

Muhtasari

• Hii itakuwa siku ya kipekee kwa mashabiki wa Bongo Fleva wa Kenya ambao kwa muda mrefu pia wamekuwa wakivutana kuhusu ubabe wa wasanii hao.

Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Image: FACEBOOK, INSTAGRAM

Kwa mara ya kwanza katika historia ya muziki wa Bongo Fleva, wasanii Alikiba na Diamond Platnumz watakuwa na shoo zao tofauti ndani ya siku moja nchini Kenya.

Wasanii hao ambao wamekuwa wakihasimiana kwa muda mrefu watakutaka kwenye udongo wa Kenya Oktoba 28.

Kwa upande wake, Diamond atakuwa anatumbuiza jijini Nairobi katika ukumbi wa Ngong Racecourse kwa tamasha kubwa la Oktoba Fest linaloandaliwa na kampuni ya kinywaji cha bia ya Tusker.

Wakati huo huo, Alikiba naye atakuwa anatumbuiza jijini Eldoret katika uzinduzi wa klabu cha starehe cha TLB ambacho kitafunguliwa Oktoba 28.

Hata hivyo, kinyume na Diamond ambaye amethibitisha kupitia kurasa zake mitanaoni kuhudhuria na kutumbuiza Oktoba Fest, Alikiba hajathibitisha kuwepo Eldoret lakini kweney ukurasa wa Instagram wa klabu hiyo ya TLB Lounge, wameweka bango la kuthibitisha kwamba msanii huyo wa Kings Music atakuwepo.

Hii itakuwa siku ya kipekee kwa mashabiki wa Bongo Fleva wa Kenya ambao kwa muda mrefu pia wamekuwa wakivutana kuhusu ubabe wa wasanii hao wawili kuhusu ni nani anafaa kutawazwa rasmi kama mfalme wa muziki huo.

Itasubiriwa kuonekana ni tamasha la msanii yupi ambalo litafurika Zaidi, licha ya kwamba matamasha hayo yatafanyika katika majiji tofauti yaliyotenganishwa na umbali wa Zaidi ya kilomita 300.