Wasioamini Mungu waitaka DCI kumkamata pasta Ng'ang'a kwa kukejeli sadaka ya Sh500

“Kutokana na ugumu wa maisha, Wakenya wengi wamepoteza matumaini katika harakati zao za kujitafutia riziki, Pasta Ng’ang’a amechukua fursa hii kuwaahidi Baraka za kimiujiza ambazo hazina mashiko" walisema.

Muhtasari

• Pia kwa wakati mmoja walidai kwamba maeneo ya ibada yanafaa kutozwa ushuru wakisema sadaka ambayo wanaikusanya haziratibiwi jinsi zinavyotumiwa.

Harrison Mumia na Pasta Ng'ang'a
Harrison Mumia na Pasta Ng'ang'a
Image: Maktaba

Jamii ya wasioamini katika uwepo wa Mungu nchini Kenya – Atheists – wametoa wito kwa idara ya upelelezi wa jinai DCI kumchukulia hatua za kisheria mchungaji mwenye utata kutoka kanisa la Neno Evangelical, James Ng’ang’a.

Kupitia barua kwa vyombo vya habari ambayo ilitiwa saini na mwenyekiti wa jamii hiyo Harrison Mumia na kuchapishwa pia kwenye ukurasa wao wa X, walidai kwamba klipu ya pasta Ng’ang’a akikejeli sadaka ya muumini mmoja ya shilingi 500 inaenda kinyume na maadili.

Wasioamini Mungu walidai kwamba kitendo cha Ng’ang’a kusema kwamba hawezi kukubali sadaka ya shilingi 500 kwa ajili ya maombi maalum kinamfanya kuwa kama mtu wa kuchangisha pesa na wala si mchungaji.

“Tunaitaka DCI kumtia mbaroni mchungaji James Ng’ang’a, ambaye tunamuona kama mchangishaji wa pesa na mkora. Pasta Ng’ang’a amekuwa na hulka ya kuwaibia waumini wasiojua na kuchukua pesa kutoka kwao kwa nguvu akijificha nyuma ya jina la Mungu na Biblia. Windo lake ni waliopoteza matumaini na maskini… anatumia miujiza bandia na kudanganya kuhusu vitendo vya roho mtakatifu visivyo na mashiko,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

“Kutokana na ugumu wa maisha, Wakenya wengi wamepoteza matumaini katika harakati zao za kujitafutia riziki, Pasta Ng’ang’a amechukua fursa hii kuwaahidi Baraka za kimiujiza ambazo hazina mashiko. Utapeli wa aina yoyote haufai kukubaliwa nchini Kenya. Tunawataka Wakenya wote kujitenga mbali na Pasta Ng’ang’a na kanisa lake,” walisema Zaidi.

Hii si mara ya kwanza kwa Atheists nchini Kenya kumulika vitendo vya kidini.

Itaumbukwa kwa wakati mmoja kukiwa na vuguvugu la kufungwa kwa sehemu za starehe zinzowasumbua watu kwa kelele usiku, jamii hiyo ilitaka pia makanisa kufungwa.

Pia waliwahi toa pendekezo la kupigwa marufuku kwa ibada za maombi shuleni na katika ofisi za kiserikali.

Pia kwa wakati mmoja walidai kwamba maeneo ya ibada yanafaa kutozwa ushuru wakisema sadaka ambayo wanaikusanya haziratibiwi jinsi zinavyotumiwa.