North Eastern ingekuwa Dubai kama viongozi wangefuata mafundisho ya Uislamu - Bon Mwangi

“Unafiki miongoni mwa Wasomali wasomi uko katika ngazi nyingine, watafanya Sala 5, na wasiwe na tatizo la kuwaibia maskini...Ukora mwingi huku wakinukuu Quran Tukufu,” Mwangi alisema.

Muhtasari

• Mwangi hata hivyo alimalizia kwa kuwalaumu wapiga kura wa eneo hilo kuwachagua viongozi wanafiki kila uchaguzi.

Kaskazini mashariki mwa Kenya na Dubai
Kaskazini mashariki mwa Kenya na Dubai
Image: Facebook//Boniface Mwangi, Visit Dubai

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu, Boniface Mwangi amewalaumu viongozi wa ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Kenya kwa kufeli wapiga kura wao.

Mwangi ambaye alikuwa anazungumzia athari hasi za mafuriko kutokana na mvua nyingi za El Nino ambazo zimeathiri maelfu ya watu katika ukanda huo, alisema kwamba viongozi wa eneo hilo ni wanafiki.

Mwanaharakati huyo alidai kwamba viongozi hao wanajifanya wachamungu hali ya kuwa wanaendelea kuibia maskini kile kidogo ambacho wanatengewa kuwanufaisha nacho.

Mwangi anahisi ukanda huo ungekuwa na kila sababu ya kujivunia mandhari mazuri iwapo tu viongozi wao wangewajibika, lakini unafiki wao kujifanya wachamungu hali ya kuwa ni mdudu fukunyuku umeliacha eneo hilo kusalia nyuma kimaendeleo kwa muda wote tangu uhuru.

Kwa mujibu wa Mwangi, ukanda wa Kaskazini Mashariki sasa hivi ungekuwa unajivunia hadhi kama ya Dubai, Doha, Ankara au hata Qatar ikiwa wangekuwa na viongozi wanaozingatia maadili na mafundisho ya Uislamu.

“Unafiki miongoni mwa Wasomali wasomi uko katika ngazi nyingine, watafanya Sala 5, na wasiwe na tatizo la kuwaibia maskini. Kaskazini Mashariki mwa Kenya ingekuwa Dubai, Doha, Qatar, au Ankara ikiwa wangefuata tu mafundisho ya Uislamu. Ukora mwingi huku wakinukuu Quran Tukufu,” Mwangi alisema.

Mwanaharakati huyo alichapisha picha za jinsi mafuriko yamezamisha nyuma na kaya kadhaa katika eneo hilo na kusema kwamba watu wa eneo hilo wanaishi kama hayawani hali ya kuwa viongozi wao wanapunja raha jijini Nairobi kila uchao.

“Watu wa North Eastern wanaishi kama wanyama na viongozi wao wanaponda raha Nairobi. Hao na watu wa Turkana, na Kilifi wako na tabia ya kuchagau viongozi wakora,” alisema.