Mimi na Diamond hatupo katika generation moja kimuziki - Alikiba

“Generation ya tatu sasa ndio kuna kina Matonya, Alikiba, Belle9, Barnaba. Ya nne sasa ndio unawakuta kina Diamond, Hussein Machozi, Marlaw,” alisema Alikiba.

Muhtasari

• Aliwataja baadhi ya wasanii waliotangulia mbele yake na kusema kwamba yeye anakuja katika kizazi toafauti na Diamond kuja baadae katika kizazi kingine pia.

Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Image: FACEBOOK, INSTAGRAM

Mkurugenzi wa lebo ya Kings Music anayetajwa kuwa mfalme wa Bongo Fleva ya kizazi kipya, Alikiba amenyoosha maelezo kwa wale wanaojaribu kumlinganisha kwa kila kitu kimuziki na Diamond Platnumz.

Akizungumza kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa kwenye boti kubwa ya kuelea baharini – Yatch – Alikiba alisema kwamba wasichokifahamu wengi ni kwamba yeye na Diamond hawapo katika kundi moja kisanii.

Msanii huyo ambaye si muongeaji sana aliamua kuwarudisha nyuma wenzake kwa kuelezea kwamba japo yeye amekuwepo kwenye tasnia kwa miaka mingi, lakini bado hajafikia kiwango cha kuitwa gwiji wa muziki wa Bongo.

Aliwataja baadhi ya wasanii waliotangulia mbele yake na kusema kwamba yeye anakuja katika kizazi toafauti na Diamond kuja baadae katika kizazi kingine pia.

“Mimi nilianza muziki nikiwa mdogo sana, ni legend ndio lakini unajua siwezi kuwa legend kabla ya wasanii kama Professor Jay, Dully Sykes, Mr Blue, hao ni malejendari kaka zetu hao,” alisema.

“Kuna kiwango unafika ndio uitwe legend, mimi generation yangu ni ya tatu. Generation ya kwanza ilikuwa ni ya kina Professor Jay, Mr 2, Kwanza Unit, generation ya pili ni ya kina Dully Sykes, Mr Blue, Juma Nature, AY, Mwana FA na wengine.”

“Generation ya tatu sasa ndio kuna kina Matonya, Alikiba, Belle9, Barnaba. Ya nne sasa ndio unawakuta kina Diamond, Hussein Machozi, Marlaw,” alisema Alikiba huku pia akimtambua Marioo kama generation inayofuata na pia kina Jay Melody.