Samidoh atangaza kuanzisha wakfu wake wa kusaidia jamii katika njia mbalimbali

Samidoh alikumbuka jinsi alipitia maisha magumu akiwa mtoto alipobaki yatima na kuweka nadhiri kwamba siku akifanikiwa kimaisha atajaribu kusaidia jamii.

Muhtasari

• Samidoh alisema kuwa kwa muda sasa amekuwa akiwashika vijana mkono katika mahitaji yako kupitia wakfu wake, Gita la Samidoh.

Samidoh
Samidoh
Image: Facebook

Msanii wa muziki wa Mugithi ambaye pia ni afisa wa polisi, Samwel Muchoki maarufu Samidoh ametangaza hafla yake kubwa itakayofanyika leo Alhamisi Novemba 30 jijini Nairobi.

Hafla hiyo itakuwa ya kuzindua wakfu wake rasmi wa kusaidia watu weney mahitaji maalum katika jamii.

Samidoh alisema kuwa kwa muda sasa amekuwa akiwashika vijana mkono katika mahitaji yako kupitia wakfu wake, Gita la Samidoh - lakini sasa ni muda mwafaka wa kuzindua wakfu kamili ili kupata nafsi nzuri ya kuwasaidia hata Zaidi.

“Katika miaka minne iliyopita, kupitia Guitar ya Samidoh Initiative, tumesaidia watu kupitia programu za Elimu, Kulisha, kutafuta na kuwasaidia wasanii wajao kurekodi muziki wao miongoni mwa shughuli nyinginezo. Na Sasa mabibi na mabwana maono yamekua makubwa na tutazindua Samidoh Foundation tarehe 30 Novemba pale Parklands sports Club,” Samidoh aliandika kwenye kadi ya mwaliko aliyochapisha katika kurasa zake mitandaoni.

Samidoh aliwaalika wafuasi wake wote ambao wamekuwa wakimuonesha upendo kupitia mitandao ya kijamii kujiunga naye katika kufanikisha jambo hilo huku pia akichukua fursa hiyo kuelezea maisha yake jinsi alivyojipata katika kaunti ya Nyandaru baada ya kuzaliwa Nakuru.

Pia alifichua masaibu ambayo amepitia tangu alipoanza kujitegemea akiwa kijana mdogo kutokana na kubaki yatima.

“Kijana huyo [Samidoh] aliyekuwa mcheshi na mwenye tabasamu alikumbana na changamoto nyingi zilizomfanya ajitegemee katika umri mdogo, lakini matumaini yake, ari na haiba yake ilivutia jamii kusaidia maisha yake ya kila siku na Elimu. Maisha yalichukua mkondo mpya. Lakini katika changamoto zake aliweka nadhiri kwamba siku moja pia ataisaidia jamii yake,” Samidoh alisema.