Terence Creative asherehekea miaka 7+ bila kuvuta sigara, bangi wala shisha

Terence kwa wakati mmoja aliwahi hadithia jinsi maisha yake yalikuwa magumu kwa kuishi na bibi yake aliyekuwa anauza pombe katika mtaa wa mabanda wa Mathare, Mlango Kubwa.

Muhtasari

• “Leo nashukuru kwa safari—kila hatua, changamoto, na ushindi umeunda vile nilivyo leo." alisema.

• Terence alishiriki msurur wa picha zake za TBT mojawapo ikiwa ambayo alikuwa anavuta sigara.

Terence Creative
Terence Creative
Image: Facebook

Mchekeshaji ambaye pia ni muigizaji Terence Creative leo hii anasherehekea miaka saba na Zaidi tangu ajikomboe kutoka kwa uvutaji wa sigara na mihadarati.

Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, Terence aliandika ujumbe mzito wa mafunzo ambayo alikabidhiwa na nyanya yake, akisema kuwa leo hii amekuwa mtu wa kuonekana japo mbele za watu kwa sababu ya kukumbatia mafunzo hayo.

Kwa mujibu wake, bibi yake alimfunza muda wote kuwa mwenye shukrani kwa Mungu, kuwa wa msaada na heshima kwa wasio nacho, lakini pia kutomuibia mtu yeyot iwe ni Amani ya nafsi, furaha au hata mali.

“Mafunzo kutoka kwa bibi yangu, 1. Kuwa na shukrani kwa Mungu kila wakati. 2. Saidia na kuwaheshimu wasiobahatika. 3. Kamwe usinyang'anye mtu yeyote amani, furaha au mali.”

“Leo nashukuru kwa safari—kila hatua, changamoto, na ushindi umeunda vile nilivyo leo. Hapa ni kukumbatia njia iliyo mbele kwa mikono wazi, 🙏🙏🙏🙏 #childofLight. Kuadhimisha miaka 7 na Zaidi bila kuvuta vilevi (hakuna bangi, sigara, shisha, nk) #NaJiniceBilaDrugs #JiniceBilaDrugs,” Terence alijipongeza.

Terence alishiriki msurur wa picha zake za TBT mojawapo ikiwa ambayo alikuwa anavuta sigara.

Itakumbukwa mchekeshaji huyo ambaye mwishoni mwa mwaka jana alipiga hatua kubwa kwa kuandaa hafla kubwa ya uzinduzi wa filamu yake ya Wash Wash 4, si mara ya kwanza amekuwa akiyazungumzia maisha yake ya zamani.

Terence kwa wakati mmoja aliwahi hadithia jinsi maisha yake yalikuwa magumu kwa kuishi na bibi yake aliyekuwa anauza pombe katika mtaa wa mabanda wa Mathare, Mlango Kubwa.