Kuanzia leo sifanyi kolabo wala remix na msanii yeyote yule, labda nirogwe - Rayvanny atania

“Binafsi nimeumizwa sana na maneno ya watu pia nimesikitishwa sana kwa kweli. Kwa hiyo mimi kama chui kuanzia leo sifanyi kolabo wala remix na msanii yeyote yule," alitania.

Muhtasari

• Kutokana na hilo, aliapa kutofanya remix au kolabo na msanii yeyote yule, akisema kwamba labda afanyiwe ulozi tu na kubadili msimamo wake.

Rayvanny
Rayvanny
Image: Facebook

Mmiliki wa lebo ya muziki ya Next Level Music, Rayvanny ametangaza kuacha kufanya kolabo na msanii yeyote yule kuanzia sasa kwenda mbele.

Hii ni baada ya kuumizwa vikali na maneno ya watu kwamba anarukia ngoma kali za wasanii chipukizi na kuwashirikisha kufanya remix kwa faida yake binafsi na wala si kuwafaidi wasanii hao ibuka.

Kupitia instastory yake, Rayvanny alisema kwamba tamko hilo limemuumiza kwa muda sasa baada ya kufanya remix kadhaa na wasanii chipukizi kama njia ya kuwaninua lakini kwa walimwengu ameonekana kama mtu ambaye anadandia ili kujinufaisha.

Kutokana na hilo, aliapa kutofanya remix au kolabo na msanii yeyote yule, akisema kwamba labda afanyiwe ulozi tu na kubadili msimamo wake.

“Binafsi nimeumizwa sana na maneno ya watu pia nimesikitishwa sana kwa kweli. Kwa hiyo mimi kama chui kuanzia leo sifanyi kolabo wala remix na msanii yeyote yule kuanzia leo yaani sitaki kusikia kabisa. Labda nirogwe,” Rayvanny alisema.

Rayvanny alisema haya japo kwa upande mwingine alionekana kutania hilo na kuwataka wasanii wanaotaka remix kumtumia mistari yao ili wafanye remix wenye wivu wajinyonge.

Hii ni baada ya kuwajibu wakosoaji wake akisema kwamba si kudandia bali ni kuchagua kwake mwenyewe tu kufanya remix ya ngoma gani kali.

Akitolea mfano, Rayvanny alisema angeamua kuchagua ngoma kali za kufanya remix basi angeendea ENJOY yake Jux na Diamond au SINGLE AGAIN yake Harmonize –ambayo alidai Harmonize aliwahi mtumia beat ili wafanye remix lakini mwenyewe hakutaka tu.