Harmonize atangaza kufunga ndoa kabla ya kufikisha miaka 30 miezi michache ijayo

Hata hivyo, Harmonize hakubainisha iwapo atamuoa mrembo mpya - Poshy Queen - ambaye wiki jana aliahidi kuwa tayari kumtolea damu na figo, au atatambulisha mrembo mwingine.

Muhtasari

• “Sitapigana vita na mtu yeyote, sina kabisa nguvu ya kujibizana. Pia ninamuombea kila mmoja wenu kushinda,” Aliongeza.

Harmonize na barafu ya moyo wake, Poshy Queen.
Harmonize na barafu ya moyo wake, Poshy Queen.
Image: Instagram

Bosi wa lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide, Rajab Abdul Kahali, maarufu kama Harmonize ametangaza mwaka huu atafunga ndoa na mwanamke ampendaye kabla ya kufikisha miaka 30.

Kupitia instastory yake, Harmonize alisema kwamba kwa muda mrefu sasa amekuwa mtu wa kujitolea kimasomaso kwa muziki kuwaridhisha kwa burudani, mashabiki wake na sasa ni muda pia wa kujitolea kwa nguvu zote katika ndoa.

Msanii huyo ambaye amekuwa akichumbiana na wanawake wazuri lakini uhusiano wao kuishia kwenye njia pand baada ya muda mfupi alisema safari hii anataka kuingia miaka 30 akiwa mwanamume mwenye ndoa yake.

“Nimekuwa serious miaka yote, ila 2024 ninataka tu kuichukua katika kiwango kingine. Katika Mungu, kimuziki lakini pia kwenye mapenzi,” Harmonize alisema.

“Nitaoa inshaallah kabla ya siku yangu ya kuzaliwa, ninataka kuvuka na kujiunga na kundi la watu wa miaka 30 nikiwa kama mwanamume mwenye ndoa,” aliongeza.

Msanii huyo pia alisema moja ya vitu ambavyo anataka kujiepusha navyo mwaka huu ni kujibizana na watu bila sababu katika mitandao ya kijamii lakini pia kwenye mahojiano ya vyombo vya habari.

“Sitapigana vita na mtu yeyote, sina kabisa nguvu ya kujibizana. Pia ninamuombea kila mmoja wenu kushinda,” Aliongeza.

harmonize
harmonize

Tangazo hilo linakuja wiki moja tu baada ya kumzindua mpenzi wake mpya kwa jina Poshy Queen.

Harmonize na Queen ambao wanaitana kwa misimbo ya Adamu na Hawa wamekuwa wakitumiana jumbe za kimahaba katika mtandao wa Instagram.

 Kwa wakati mmoja, Harmonize alionesha kuridhika na penzi la mprembo huyo anayetajwa kuwa mpenzi wa zamani wa aliyekuwa DJ wa Harmonize, alimwambia kwamba yuko radhi kabisa kumtolea damu na hata figo.

“Sio tu damu, hata figo nakutolea Eva wangu. 2017 na sasa tuko hapa. Ni historia iliyoje kuwaambia wanetu Nova na Zuuh Konde, ni sharti wawe wastahimilifu. Mapenzi ni ukichaa,” Diamond alimjibu.

Hata hivyo, katika tangazo hilo lake la kuoa, hakuweka wazi kama atamuoa mwanamke huyo mpya au atamtambulisha mwanamke mwingine – maana kwa Harmonize kuwatambulisha warembo wapya kila uchao si jambo la kushangaza.