Harmonize na Diamond kugongana Ijumaa hii

Harmonize alikuwa chini ya uongozi wa Diamond hadi mwaka 2019 alipoondoka kwa njia ya kishari kupelekea wawili hao kuanza kuchukiana.

Muhtasari

• “Mwaka huu si mpya tena, tuonane Ijumaa,” Harmonize aliandika kwenye picha yake, Shmurda na Bien.

Diamond na Harmonize
Diamond na Harmonize
Image: Facebook

Baada ya Harmonize kutangaza kwamba Ijumaa hii atakuwa na jambo lake kubwa, msanii Diamond naye amedakia tarehe hiyo hiyo na kutangaza kuwa atakuwa na jambo la kwake.

Harmonize alikuwa wa kwanza kutangaza kwamba Ijumaa hii ya Januari 26, ambapo alifichua kuachia kolabo yake iliyosubiriwa kwa hamu na ghamu na mashabiki wake.

Harmonize alisema ataachia kolabo yake ya ‘I Made It’ Ijumaa, wimbo ambao amemshirikisha rapa wa Marekani Bobby Shmurda na msanii wa Kenya Bien Sol Baraza.

“Mwaka huu si mpya tena, tuonane Ijumaa,” Harmonize aliandika kwenye picha yake, Shmurda na Bien.

Saa chache baadae, Diamond naye ambaye amekawia kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, isipokuwa tu kwenye stories, alichapisha picha ya ndege aina ya helikopta ikiwa inapeperushwa bango lenye ujumbe wake.

Katika ujumbe huo, Diamond alisema kwamba Ijumaa, Januari 26 atakuwa na jambo lake kuu, jambo haijulikani ni jambo gani hilo ambalo atalizindua.

“Januari 26 – Diamond Platnumz,” bango hilo lilisomeka.

Wasanii hao wawili ambao wamekuwa wakihasimiana na kutupiana vijembe kwa muda wamekuwa wakionesha ushindani katika kila jambo, japo baadhi ya watu wanahisi kwamba hakuna uadui baina yao Zaidi tu na kuchangamsha genge.

Harmonize alikuwa chini ya uongozi wa Diamond hadi mwaka 2019 alipoondoka kwa njia ya kishari kupelekea wawili hao kuanza kuchukiana, kila mmoja akijitahidi kumzungumzia mwenzake kwa mabaya.