Akademia ya soka ya Michael Olunga yafadhili wanafunzi 28 kujiunga kidato cha kwanza

Wavulana 28 wenye talanta kutoka kwa familia zenye uhitaji watasoma chini ya taasisi yake hadi watimize ndoto zao.

Muhtasari

• Zaidi ya hayo, mhandisi huyo alifadhili wavulana wengine 5 walio na umri wa chini ya miaka 15 katika Shule ya St. Joseph's Rapogi.

MOFA
MOFA
Image: FACEBOOK//MOFA

Mshambuliaji wa timu ya Al Duhail SC ya nchini Qatar, Michael Olunga kupitia kwa academia yake ya soka ya MOFA amefanikiwa kuwafadhili vijana wa chini ya umri wa miaka 15 wapatao 28 kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali mkoani Nyanza.

Hili liliwekwa wazi kupitia kwa ukurasa wa Facebook wa MOFA ambapo Olunga alijitolea kimasomaso kuwafadhili vijana hao wenye talanta kuendeleza masomo yao katika shule za upili.

Mzaliwa wa Kaunti ya Homabay, ni mhandisi wa kulipwa anayecheza nchini Qatar katika klabu ya Al Duhail SC kama fowadi ambapo amejizolea umaarufu sio tu nchini Kenya na Qatar bali pia katika ulimwengu wa soka duniani.

Kupitia taasisi yake ya MOFA, aliwapeleka wavulana 10 chini ya miaka 15 katika Shule ya Upili ya Bweni ya Kisumu Day, na wavulana 13 walio chini ya umri wa miaka 15 huko St. Mary's Yala, Kaunti ya Siaya.

Zaidi ya hayo, mhandisi huyo alifadhili wavulana wengine 5 walio na umri wa chini ya miaka 15 katika Shule ya St. Joseph's Rapogi.

Wavulana 28 wenye talanta kutoka kwa familia zenye uhitaji watasoma chini ya taasisi yake hadi watimize ndoto zao.

Olunga alianzisha akademia yake ya soka miaka michache iliyopita lakini katika kipindi hicho, MOFA imejizolea umaarufu na kukuza vipaji ainati katika soka la Kenya.