Guardian Angel atetea hatua ya wainjilisti wa kisasa kusuka rasta

"Kujitolea kwangu kwa mke wangu kunaenda Zaidi ya umri na maoni ya watu. Kwa sababu mkiingia kwa hicho kitanda ni wewe na mke wako, hamna jamaa wa maoni hapo." alisema.

Muhtasari

• "Kuna watu ambao walioana mimi nikianza kudate mke wangu na wako na huo umri tunaongelea na sasa hivi hawako pamoja."

• Angel ambaye pia ana rasta alisema kwamba Mungu haangalii jinsi mtu alivyo kwa nje bali anazingatia Zaidi kiichoko ndani yake lakini pia matendo yake duniani.

Muimbaji wa injili amesema si vibaya kuwa na rasta
Guardian Angel// Muimbaji wa injili amesema si vibaya kuwa na rasta
Image: Facebook

Msanii wa injili kutoka Kenya, Guardian Angell ametetea hatua ya wainjilisti wa kizazi cha sasa kuwa na nywele aina ya rasta – jambo ambalo linaonekana kwenda kinyume na kanuni za kihafidhina zilizowekwa na wainjilisti wa siku za nyuma kabla ya ujio wa utandawazi na usasa.

Akizungumza Jumapili nchini Tanzania katika ibada ya mchungaji kwa jina Nabii Malisa inayopeperushwa moja kwa moja kwenye runinga ya Wasafi, msanii huyo alisema kwamba kuwa na rasta hakumaanishi kwamba mtu hajapata wokovu.

Angel ambaye pia ana rasta alisema kwamba Mungu haangalii jinsi mtu alivyo kwa nje bali anazingatia Zaidi kiichoko ndani yake lakini pia matendo yake duniani.

Mwinjilisti huyo aliweka wazi kwamba kwa uelewa wake wa neno, kama Mungu angekuwa anaangalia muonekano wa mtu kabla ya kumteua kulitangaza neno lake basi kila mtu katika injili angekuwa ni kipara.

Kuwa na rasta sio shida ukiwa na Mungu, kama Mungu angeona kuwa na nywele ni dhambi basi wote tungekuwa vipara tu,” Angel alisema.

Awali katika mahojiano kwenye runinga ya Clouds, mtumishi huyo wa Mungu alitetea ndoa yake ambayo imepata pingamizi kali kutoka kwa baadhi ya watu kutokana na kigezo cha upana wa umri baina yake na mke wake Esther Musila.

 Angel alisema kwamba kigezo cha kumuoa mwanamke anayemzidi kwa umri wa miaka 20 hakina msingi kwani kunao wengi waliooana wakiwa na umri sawa na wakaishia kuachana, lakini wao licha ya utofauti mkubwa kiumri, bado wako pamoja miaka miwili baadae tangu kuoana.

"Kama umri ndio the kigezo muhimu cha kuzingatia, kuna watu wengi wameoana hivyo na wameachana muda si mrefu. Kuna watu ambao walioana mimi nikianza kudate mke wangu na wako na huo umri tunaongelea na sasa hivi hawako pamoja."

 

"Kujitolea kwangu kwa mke wangu kunaenda Zaidi ya umri na maoni ya watu. Kwa sababu mkiingia kwa hicho kitanda ni wewe na mke wako, hamna jamaa wa maoni hapo. Mimi ilmradi tu nina furaha kwenye ndoa yangu, hiyo ndio muhimu. Wewe kwanza si wetu, nilikupata tu Nairobi sasa hisia zako zinanihusu na nini?" Angel aliwafokea wanaokosoa ndoa yake.