Makanisa yamejaa usanii, wachekeshaji wanapewa muda mwingi kuliko mahubiri - Burale

“Hata baadhi ya miziki ya injili inaweza ikamfanya shetani mwenyewe kubaki kinywa wazi. Ni lazima miziki hii ikashifiwe hadharani." Burale alisema.

Muhtasari

• “Usanii mwingi sana umeingia kanisani… hatufai kutoa muda wa dakika 30 kwa wachekeshaji kuchekesha waumini kwa vichekesho chafu" alisema.

Image: INSTAGRAM//ROBERT BURALE

Robert Burale amezua maoni kinzani baada ya kudai kwamba makanisa mengi ya kizazi cha leo yanawapa muda mwingi wachekeshaji kutumbuizia waumini muda wa mahubiri.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Israel Robert Burale alisema kwamba usanii mwingi umeingizwa kanisani na baadhi ya wachekeshaji wanatumia muda wa mahubiri kuchekesha waumini kwa kutumia vichekesho chafu wakinukuu Biblia visivyo.

“Usanii mwingi sana umeingia kanisani… hatufai kutoa muda wa dakika 30 kwa wachekeshaji kuchekesha waumini kwa vichekesho chafu (wakati mwingine wakitumia maandiko) wakati wa ibada kuu. Watu wanataka kuhubiriwa kuhusu Yesu kutokana na sababu mbalimbali,” Burale alisema.

Mhubiri huyo ambaye pia anajulikana sana kwa mikutano yake ya ushauri nasaha na jumbe za kutia moyo kwa umati alisema kwamba hata baadhi ya watu wanaojitambulisha kama wanamuziki wa injili na miziki yao inaweza ikamshangaza hata shetani mwenyewe, kwa jumbe zao zisizostahili kuingia kanisani.

Burale aliwashauri waumini na wachungaji wenzake kwamba ni muda sasa wa kutenganisha mbivu na mbichi ili kuliunda jeshi aminifu kwa Mungu kwa ajili ya nyakati za mwisho.

“Hata baadhi ya miziki ya injili inaweza ikamfanya shetani mwenyewe kubaki kinywa wazi. Ni lazima miziki hii ikashifiwe hadharani. Tunahitaji kuandaa jeshi la nyakati za mwisho… na hili linahitaji bidii na utiifu,” Burale alimaliza.