Don Jazzy aeleza sababu ya kuuza hisa nyingi ya lebo yake kwenda kwa Universal Music Group

Lebo hiyo ya Don Jazzy inajivunia kuwatoa wasanii wakubwa wanaoiteka Afrobeats ndani na nje ya bara la Afrika wakiwemo Rema, Ayra Starr, Johnny Drille miongoni mwa wengine wengi.

Muhtasari

• "Wapendwa wa Mavin Family, nina furaha kutangaza kwamba Mavin Records imeshirikiana na Universal Music Group, kuashiria ukurasa mpya katika safari yetu." Jazzy alisema.

Don Jazzy auza zaidi ya nusu ya hisa za Mavin Records
Don Jazzy auza zaidi ya nusu ya hisa za Mavin Records
Image: Instagram

Don Jazzy, ambaye ni mmiliki wa lebo ya muziki yenye ufanisi mkubwa barani Afrika – Mavin Records – amevunja ukimya wake baada ya kubainika kwamba hisa karibia zote za lebo hiyo zimeuzwa kwa kampuni ya kimataifa ya muziki, Universal Music Group.

UMG katika taarifa iliyotolewa Jumatatu Februari 26, 2024 ilisema mpango huo unasalia chini ya idhini ya udhibiti na unatarajiwa kufungwa mwishoni mwa robo ya tatu ya mwaka 2024.

Mkataba huo utawafanya mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mavin Don Jazzy na COO Tega Oghenejobo waendelee kuiendesha kampuni hiyo, ilisema taarifa.

Akithibitisha Universal Music Group kama mmiliki wa hisa nyingi katika Mavin Records, Don Jazzy aliandika;

"Wapendwa wa Mavin Family, nina furaha kutangaza kwamba Mavin Records imeshirikiana na Universal Music Group, kuashiria ukurasa mpya katika safari yetu. Ushirikiano huu ni hatua muhimu ambayo inatambua talanta yetu ya pamoja na bidii, inayolenga kuinua muziki wa Kiafrika kwenye jukwaa la kimataifa.”

“Ushirikiano wetu na UMG utaleta muziki zaidi, uvumbuzi, na fursa, kutuwezesha kuonyesha vipaji vya Kiafrika duniani kote. Tunapoanza njia hii mpya ya kusisimua, dhamira yetu ya msingi na maadili yatabaki kuwa sawa, kuhakikisha kwamba kiini cha Mavin na kujitolea kwetu kusukuma mipaka ya muziki kunaendelea kustawi.”

“Hatua hii ya kusonga mbele ni uthibitisho wa kujitolea kwa wasanii wetu, wafanyikazi, na, muhimu zaidi, ninyi, mashabiki wetu, ambao uungwaji mkono wao usioyumba umekuwa muhimu katika kufikia wakati huu. Kwa pamoja, tunatazamia kutengeneza historia, kuvunja rekodi zaidi, na kujenga urithi wa kudumu.”

“Asante kwa kuendelea kutuamini. Hapa ni kwa mustakabali wetu mzuri pamoja,” alimaliza.

Lebo hiyo ya Don Jazzy inajivunia kuwatoa wasanii wakubwa wanaoiteka Afrobeats ndani na nje ya bara la Afrika wakiwemo Rema, Ayra Starr, Johnny Drille miongoni mwa wengine wengi.