Ndoa yangu imekuwa na hali mbaya tangu Juni mwaka jana - Jackline Wolper afichua

Alifunga ndoa na mume wake Rich Mitindo Novemba 2022, lakini amefichua kwamba mwezi Juni 2023, kitumbua cha ndoa yake kiliingia mchanga na amekuwa akilia na kufuta machozi.

Muhtasari

• "Mimi toka Juni mwaka jana siko vizuri katika ndoa yangu. Kuanzia mume wangu yuko China, siko naye vizuri kiukweli,” Wolper aliongeza.

Wolper afunga ndoa na mume mpya
Wolper afunga ndoa na mume mpya
Image: Instagram

Mwigizaji lejendari wa fillamu za Bongo, Jackline Wolper amefichua kwamba amekuwa akipitia hali ngumu sana katika ndoa yake kwa Zaidi ya miezi 9 sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Wolper alifichua kwamba japo ndoa yake imekuwa na hali ngumu tangu Juni mwaka jana, yeye si mtu rahisi kuanika mambo yake mitandaoni, hivyo kuifanya kuwa vigumu kwa watu kupata umbea wa ndoa yake.

Alikiri kwamba ni kweli yeye na mume wake Rich Mitindo hawayakuwa katika maelewano mazuri tangu Juni, ikiwa ni miezi kama 7 tu baada ya kufunga ndoa.

“Ni kweli kuna vitu vinanivuruga lakini mimi huwa sichapishi vitu hivyo. Mimi vitu vimenivuruga toka mwezi wa 6 mwaka jana siko sawa na mume wangu ndani, lakini sijawahi post popote. Mimi huwa ni mtu ambaye nimenyoosha maelezo.”

“Na kwa wale ambao wanafuatilia mambo yangu nafikiri mtakuwa mnajua, mimi toka Juni mwaka jana siko vizuri katika ndoa yangu. Kuanzia mume wangu yuko China, siko naye vizuri kiukweli,” Wolper aliongeza.

Mama huyo wa watoto wawili alieleza kwamba ameshakua na kuna vitu vingine ambavyo hawezi kuvifanya, kama vile kukurupuka mitandaoni kuhusu masuala ya ndani ya ndoa yake.

“Kuna vitu ukishakuwa lejendari, ukishakuwa mama, ukishakuwa mke, inabidi uachane navyo kwa sababu hata kikitokea ukimuuliza mtu anakuambia hii ni nyeusi wakati wewe unaiona nyekundu. Kwa hiyo kwenye maisha ya sasa hivi, kuna magonjwa kama mshtuko wa moyo, mtu unaweza ukafa mara moja ukawaacha watoto wako kisa mtu ameku’stress. Hicho kitu kiukweli mimi nilishakikataa,” alisema.

Mama P, kama anavyojiita alifunga ndoa na mume wake Rich Mitindo, mjasiriamali wa fasheni mwezi Novemba mwaka 2022, lakini amefichua kwamba mwezi Juni 2023, kitumbua cha ndoa yake kiliingia mchanga lakini amekuwa akilia na kufuta machozi pasi na watu kujua.