Nyota Ndogo ajitetea kupokea chakula kutoka kwa Hassan Joho

“Chakula kilikuwa kwa sababu ya mfungo wa Ramadan, hakikuwa chakula cha misaada, hakikuwa chakula cha kupatia wasiojiweza." alisema Nyota.

Muhtasari

• "Joho aliona wacha nipeane futar kwa ajili ya Ramadan, watu waliofunga sio watu wasiojiweza,” alifafanua Nyota Ndogo.

Nyota Ndogo.
Nyota Ndogo.
Image: facebook

Msanii wa muda mrefu Nyota Ndogo kutoka kaunti ya Taita Taveta amejitetea vikali dhidi ya kushtumiwa kupokea chakula kutoka kwa gavana wa zamani wa Mombasa, Ali Hassan Joho.

Nyota Ndogo alikuwa miongoni mwa Waislamu waliopokea chakula kilichokuwa kikisambazwa na Joho katika kaunti ya Taita Taveta, na hilo liliwavutia wengi kumshtumu kwamba hakustahili kupokea cakula hicho kwani kilikusudiwa kwa watu wasiojiweza wakati wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadani.

Hata hivyo, katika mahojiano kwa njia ya simu kupitia kituo kimoja cha redio humu nchini, Nyota Ndogo alisema kwamba asingekataa kupokea chakula hicho kwani hakikusudiwa kuwa msaada kwa maskini bali kilikuwa ni chakula kwa Waislamu wote waliofunga.

“Chakula kilikuwa kwa sababu ya mfungo wa Ramadan, hakikuwa chakula cha misaada, hakikuwa chakula cha kupatia wasiojiweza. Joho aliona wacha nipeane futar kwa ajili ya Ramadan, watu waliofunga sio watu wasiojiweza,” alifafanua Nyota Ndogo.

Akifafanua kuhusu kuitwa tajiri ambaye hastahili kupokea chakula, Nyota Ndogo alisema kwamba ni umbea na roho mbaya tu na kusema kwamba hakuna hata siku moja anakumbuka aliwahi jitangaza kuwa yeye ni tajiri.

“Watu waache roho mbaya na hakuna siku nishawahi jitangaza kwamba mimi ni tajiri, ama niko na pesa. Ningekuwa nina pesa ningepika chapatti pale siku mzima,” alisema.