Nyota Ndogo alia kwa uchungu baada ya kuambiwa mtoto si wa mumewe, ni wa mpishi wa chapati

Mwimbaji huyo alisema licha ya mtoto wake kuwa na ngozi nyeusi, mumewe ameridhika sana kupata mtoto wa Kiafrika.

Muhtasari

•Alilalamika kuwa baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakizua shaka kuhusu baba halisi wa mtoto wake wa kiume

•Alilalamika kuhusu jinsi mtumiaji wa mitandao alivyoibua madai kwamba baba halisi wa mtoto wake ni mfanyikazi wake mmoja.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwimbaji mkongwe wa Kenya Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amelalamika kihisia kuhusu unyanyasaji wa mitandaoni, wiki chache tu baada ya kujifungua mtoto wake wa tatu.

Katika video iliyojaa hisia ambayo alishiriki kwenye ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo mzaliwa wa pwani alilalamika kwamba baadhi ya watumiaji wa mtandao wamekuwa wakimdhihaki yeye na mtoto wake mchanga.

Alilalamika kuwa baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakizua shaka kuhusu baba halisi wa mtoto wake wa kiume wakidai kuwa mume wake mzungu sio baba halisi.

“Hamjambo ndugu zangu popote mlipo. Natumai nyote hamna neno. Mko wazima kabisa. Ningependa niseme kitu. Sijui kama watu wenye wako kwenye social media, yaani unaposhika simu yako wewe kwenye social media unapoandika kitu ama kumtukana mtu ambaye humjui, unamrushia matusi, unamwambia maneno ya kuudhi. Sijui kama mwajua huwa tunacatch feelings ama ni vipi,” Nyota Ndogo alilalamika kwenye video hiyo huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

Aliendelea kulalamika kuhusu jinsi mtumiaji wa mitandao alivyoibua madai kwamba baba halisi wa mtoto wake ni mfanyikazi wake mmoja.

“Mimi huwa sijali mambo mengi ambayo huwa mnayaongea. Lakini kama kuna kitu ambacho kimeniuma ni pale mtu anapokuja kwenye ukurasa wangu na kusema kwamba mimba niliyoibeba ni ya mpika chapati. Yaani mimba yangu sio ya mume wangu, ni ya mpishi wa chapati,” alisema.

Mama huyo wa watoto watatu hata hivyo alipinga madai hayo akibainisha wazi kuwa yeye mwenyewe ndiye hujitayarishia chapati katika hoteli yake.

“Chapati zenyewe nazipika mimi. Nachomeka matiti siku nzima nauzia watu chapati alafu mtu kuna kokote anakuja anasema hiyo mimba, kama mtoto ni mweusi basi ni ya mpika chapatti wangu. Haya, najitia mimba mimi ama vipi wenzangu,” alisema.

Kufuatia hayo, mwimbaji huyo mkongwe aliwataka watu kuwa waangalifu na wenye kujali hisia za watu wanapotoa maoni yoyote kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za watu.

Pia aliweka wazi kuwa mume wake mzungu ana furaha na kuridhika na mtoto wao kwani licha ya kuwa na ngozi nyeusi, wanafanana.

"Baba mwenyewe amefurahi amepata mtoto wa Kiafrika," alisema.

Huku akishiriki habari za kuzaliwa kwa mtoto wake mwezi uliopita, Nyota Ndogo alichapisha picha ya mtoto mchanga kwenye kurasa zake mtandao wa kijamii na kumtaja kama mrithi wake.

Mwimbaji huyo hata hivyo alielezea wasiwasi wake kuhusu sura ya mtoto huyo wake akidai kuwa hafanani na mzazi mwenzake.

"Karibu nyumbani mwanangu, ila hii rangi sinitaambiwa nimechiti, yani umeamua nywele ndio uchukue ya baba rangi ndio hii yetu, karibu abdalla.(URITHI TUNAO)."

Mtoto mchanga wa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ni wake wa kwanza na mume wake mzungu, Bw Henning Neilsen.