Otile Brown aeleza sababu ya kutotoa mchango wa pesa kwa mazishi ya Brian Chira

Otile pia alionekana kujitetea kwa kutotoa mchango wa fedha akisema hata kutokea kwake tu na kutumbuiza waombolezaji pasi na kuhitaji malipo ni mchango tosha na ambao unafaa kutambuliwa.

Muhtasari

• Otile Brown Jumanne alitumbuiza kibao chake cha ‘One Call’ katika hafla ya kumuaga Brian Chira.

Otile Brown
Otile Brown
Image: Screengrab

Msanii wa kizazi kipya, Otile Brown amekiri kwamba hakutoa mchango wowote wa kifedha katika safari ya mwisho ya tiktoker Brian Chira.

Akizungumza na bogu moja ya habari za burudani, Otile alionekana kujuta kutompa nyanya ya Chira mchango wowote wa kifedha licha ya kufika Githunguri kwa ajili ya mazishi na hata kupata fursa ya kutumbuiza, japo kidogo.

Alisema kwamba anafikiria kutafuta namba ya nyanya huyo ili kumtumia kitu, lakini akasisitiza kwamba atafanya hivyo iwapo atafahamishwa kama kweli ana hitaji la msaada wa kifedha.

“Siwezi dnaganya, sikutoa kitu, sijui lakini nadhani kwa sababu hiyo nahitaji kupata namba yangu na nione kama nitaweza kusaidia kwa njia moja au nyingine. Lakini hiyo ni kama ana hitaji la kipekee, kwa sababu tayari Wakenya wameshatekeleza wajibu wao,” Otile Brown alisema.

Hata hivyo, Otile pia alionekana kujitetea kwa kutotoa mchango wa fedha akisema hata kutokea kwake tu na kutumbuiza waombolezaji pasi na kuhitaji malipo ni mchango tosha na ambao unastahili kupongezwa.

Aliwashauri watu kuondoka katika hali ya kuona maisha kutoka kwa upande wa pesa katika kila kitu, na kusema kwamba kuna vitendo vingine ambavyo vinafanywa kwa moyo wa upendo ambavyo vinazidi kiasi chochote cha pesa.

“Lakini unajua hata kutokea kwangu ni jambo la maana pia, acha tuache kupunguza maisha na kuyafanya kuwa ni kuhusu pesa tu. Wakati mwingine hata kutokea tu ni mchango mkubwa sana, nimetoa mchango wangu katika njia moja au nyingine.

“Hata hivyo, simaanishi kwamba sitaki kutoa mchango, mimi sina tatizo na hilo lakini, sisi kama Wakenya tutaona chenye tutafanya, na ninachukua nafasi hii kushukuru kila mtu aliyechangia, lakini pia mimi kama nitahitajika, nitajitokeza,” alisema.

Otile Brown Jumanne alitumbuiza kibao chake cha ‘One Call’ katika hafla ya kumuaga Brian Chira, hatua ambayo alisema ilichochewa na mashabiki kumpa presha ya kutumbuiza wakidai kibao hicho kilikuwa pendwa kwa Chira.