Mahakama ya Nigeria imemfunga miezi 6 jela cross-dresser Bobrisky kwa kurarua noti ya Naira

Bobrisky, mwanamume aliyebadili jinsia na kuwa mwanamke kupitia msururu wa sajari alifungwa miezi 6 baada ya video kumuonesha akirusha noti za Naira juu klabuni kwa mashabiki wake huku akirarua zingine.

Muhtasari

• Awali iliripotiwa kwamba Bobrisky alikamatwa Jumatano iliyopita jioni na wafanyakazi wa Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC) katika Jimbo la Lagos.

Bobrisky
Bobrisky
Image: Instagram, Hisani

Mahakama Kuu ya Shirikisho huko Lagos nchini Nigeria mnamo Ijumaa asubuhi ilimhukumu mwanasosholaiti maarufu Idris Okuneye anayejulikana zaidi kama Bobrisky kifungo cha miezi sita bila chaguo la kutozwa faini kwa matumizi mabaya ya sarafu ya nchi hiyo – Naira.

Awali iliripotiwa kwamba Bobrisky alikamatwa Jumatano iliyopita jioni na wafanyakazi wa Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC) katika Jimbo la Lagos.

Haya yalithibitishwa na msemaji wa shirika hilo, Bw Dele Oyewale katika mazungumzo ya simu na jarida la SaharaReporters.

Kulingana na msemaji wa EFCC, Bobrisky alikamatwa kwa uraruaji wa noti za naira na sio kwa mtindo wake wa maisha kama mbadilishaji nguo.

"Ni kweli wavulana wetu walimkamata jana jioni huko Lagos kwa kurarua naira. Hatuna chochote cha kufanya na mtindo wake wa maisha (kuwa cross-dresser). Alishukiwa kufanya uhalifu wa kiuchumi na hiyo ndiyo sababu ya kukamatwa kwake,” Oyewale alieleza.

Kukamatwa kwa Bobrisky kulikuja saa 24 tu baada ya Jeshi la Polisi la Nigeria kusema kwamba lilikosa ushahidi wa kutosha wa kumkamata kwa kufanya mapenzi ya jinsia moja.

Jeshi la Polisi la Nigeria Jumanne iliyopita lilisema halingeweza kumkamata Bobrisky kutokana na wito wa kumkamata mhusika.

Kumekuwa na wito wa kukamatwa kwa Bobrisky, haswa baada ya mwanablogu Martins Vincent Otse, maarufu kwa jina la VeryDarkMan katika video za hivi majuzi kulaani tuzo ya Mwanamke Aliyevaa Bora kwa mwanadada huyo katika hafla ya Nollywood.

Baada ya kukamatwa, Bobrisky alishtakiwa mahakamani na EFCC kwa uhalifu unaopakana na makosa sita, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya noti za naira na utakatishaji fedha.

Klipu na picha za mwanadada huyo mwenye utata kwenye mitandao ya kijamii akifungwa pingu na kuondolewa baada ya hukumu yake kusomwa mahakamani zimesambaa mitandaoni.

Wengi wameshutumu kufungwa kwa Bobrisky kuwa ni ukosefu wa haki, huku wengi wakipongeza kuwa ni kizuizi mwafaka kwa tishio linaloongezeka la ushoga katika jamii.