Christina Shusho amkumbuka Osinachi aliyedaiwa kufa kwa kuithamini ndoa kuliko maisha yake

Ikumbukwe ilidaiwa Osinachi alisemekana kuchagua kufia kwenye ndoa ya manyanyaso kwa kuogopwa kuachwa na kuchekwa kwa kupoteza ndoa. Shusho juzi amedaiwa kukiri kuacha ndoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu.

Muhtasari

• Shusho hivi majuzi aligeuka gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukiri kwamba hayupo kwenye ndoa yake.

• Itakumbukwa msanii huyo aliyekuwa maarufu kwa wimbo ‘Ekwueme’ alidaiwa kufa kwa kipigo cha mumewe.

Christina Shusho
Christina Shusho
Image: Maktaba

Christina Shusho, msanii tajika wa injili kutoka Tanzania amemkumbuka msanii marehemu kutoka Nigeria, Osinachi Nwachukwu aliyefariki miaka miwili iliyopita mwezi kama huu wa Aprili.

Shusho alisema kwamba leo ameamua kumkumbuka Osinachi kwa njia ya kipekee kwani ni nyota wa nyimbo za injili ambaye aliashindwa kufanya maamuzi ya kumfaa, hali ambayo baadae ilikuja kumgharimu maisha yake.

“Miaka Miwili mwezi kama huu wa Nne tulimpoteza Jemedari wa Mziki wa Injili Nigeria Osinachi Nwachukwu. Leo nimemkumbuka sana na yaliyotokea mpaka mauti yalipo mkuta. Kwa Mtini Jifunzeni,” Shusho aliandika.

Itakumbukwa msanii huyo aliyekuwa maarufu kwa wimbo ‘Ekwueme’ kifo chake kilikuwa na simulizi kadha, ambazo zote zilikuwa zinaelekeza kwamba alifariki kutokana na manyanyaso kutoka kwa mume wake.

Taarifa kipindi hicho zilidai kwamba Osinachi ambaye alikuwa mke wa mwanamume mwenye cheo kanisani alitaka mara kadhaa kuiasi ndoa lakini kila mara alipokuwa anauliza ushauri kutoka kwa viongozi wa kanisa, walimsuta na kumwambia kwamba atadhalilika na kuchekwa kwa kushindwa na ndoa hali ya kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu.

Ushauri huu ulimgubika ndani ya ndoa yenye manyanyaso hadi mwishowe akaja kufariki kwa kile kilitajwa kuwa ni kipigo kutoka kwa mumewe, ambaye alikuwa anajificha kwenye kivuli cha kanisa.

Baada ya kifo chake, watoto wake pia walitilia mkazo kuwa baba yao alikuwa anampiga mama yao mara kwa mara na hadi anakata roho ni kwasababu alikuwa ametoka kupigwa muda mfupi.

Sasa, kutokana na mazingira haya yanayozunguka kifo cha Osinachi, yanaturudisha kwa Shusho ambaye pia siku za hivi karibuni ameonekana kugusia maisha katika ndoa yake.

Shusho hivi majuzi aligeuka gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukiri kwamba hayupo kwenye ndoa yake.

Kwa maelezo yake, alisema kwamba alilazimika kuiacha ndoa ili kupata muda mzuri wa kumtumikia Mungu, akionekana kuashiria kwamba pengine ndoa ilikuwa kikwazo katika huduma yake.

Hata hivyo baada ya kusemwa sana mitandaoni, Shusho alidokeza pia kuwa huenda kuna mengine Zaidi yaliyompelekea kuacha ndoa yake akisema;

Usilo lijua ni kama Usiku wa Kiza. Sio Kila kitu ni cha Kujibu na Siku ikifika ya Kuongea nitaongea.”

Kutokana na kauli hii, wengi wanahisi kwamba kunayo sababu za ndani Zaidi zilizomfanya kutoka kwa ndoa na sasa kila mmoja anasubiri muda huo kufika ili kusikia Zaidi kutoka kwake.