Mrembo aliyedaiwa kupewa Range Rover na Harmonize akiri kupenda wazee miaka 50 na zaidi

"Kwa kifupi vijana sio ladha yangu, labda aje mtu wa kuanzia 50. Kwa sababu akili yangu, mimi nimetoka kimapenzi na watu wazima sana, kwa hiyo akili yangu ni ya kiutu uzima sana," alisema.

Muhtasari

• Pia alifichua kwamba ladha yake haipo katika wanaume ambao ni wasanii, akisema kwamba haijawahi muingia katika akili zake na wala haitokuja kutokea.

Sishkiki amtaja aliyemnunulia Range Rover.
Sishkiki amtaja aliyemnunulia Range Rover.
Image: Instagram

Mjasiriamali wa kuuza nguo za wanawake Sishkiki Sikamatiki kutoka nchini Tanzania, mrembo ambaye miezi kadhaa iliyopita alisemekana kuwa mpenzi mpya wa msanii Harmonize amefichua kwamba yeye katu hawezi kuingia katika mapenzi na mwanamume wa rika lake.

Sishkiki katika mahojiano na Wasafi, alisema kwamba ladha yake ipo kwa wanaume ambao umri wao umekwenda sana, kuanzia miaka 50 na Zaidi.

Pia alifichua kwamba ladha yake haipo katika wanaume ambao ni wasanii, akisema kwamba haijawahi muingia katika akili zake na wala haitokuja kutokea.

“Wasanii sio ladha yangu, tunakutana tu kwa vitu vingine lakini si kimapenzi. Mimi sijawahi toka na siwezi toka kimapenzi na msanii. Sio kwa ubaya lakini sivutiwi na wao. Lakini wasanii wengi ni marafiki zangu.”

“Na sio kwamba ni wasanii tu, lakini pia mimi sivutiwi na vijana. Kwa kifupi vijana sio ladha yangu, labda aje mtu wa kuanzia 50. Kwa sababu akili yangu, mimi nimetoka kimapenzi na watu wazima sana, kwa hiyo akili yangu ni ya kiutu uzima sana na hivyo nikitoka na mtu kijana inakuwa kama nimemzidi kimawazo,” alieleza sababu zake.

Mrembo huyo pia aliweza kuzungumzia uhusiano wake na Harmonize, miezi kadhaa baada ya kudaiwa kupewa zawadi ya gari aina ya Range Rover na bosi huyo wa Konde Gang.

“Ningekuwa na uhusiano naye mngejua tu, yule ni mtu ambaye anapenda kuweka mahusiano yake hadharani. Kama sisi wote hatujawahi kufanya hivyo, jua kwamba tulikuwa tunataka kuchangamsha tu Instagram, si unajua. Hakuna kingine.”

“Ni ushikaji tu, unajua sisi kuwa wapenzi haiwezekani kwa kuwa ni watu wawili tofauti. Yeye ametokea dunia nyingine tofauti kimawazo na mimi vile vile. Tunakutana tu kwa ajili ya urafiki lakini kimapenzi hapana,” Sishkiki alisema.

Mwezi Machi mwaka jana baada ya uvumi kuzagaa mitandaoni kwamba Harmonize ndiye aliyemzawadi Range Rover ya rangi ya waridi, mrembo huyo alijitokeza na kukanusha vikali akisema aliyempa ni mtu mwingine tofauti huku akisisitiza Harmonize kuwa ni rafiki tu.

“Harmonize ni mshikaji wangu, mwanangu kabisa. Tunajuana muda mrefu, ni mtu mzuri sana. Sitaki kuchokonolewa na lile Range Rover nilipewa na mtu anayenidhamini sana. Ila hapo kwa ni nani, sina maoni,” Sishkiki alisema.