SisiKwaSisi: Eric Omondi afichua kuchangisha zaidi ya Ksh 72m tangu aanze kusaidia watu

Alianza kuwarai watu kuchangisha chochote kidogo walicho nacho kuwasaidia wenzao miezi 7 iliyopita, na tayari ameshagusa nyoyo za watu 68 wenye mahitaji mbalimbali.

Muhtasari

• “Tunaenda kuunda mfumo ambao utawezesha kusaidia Wakenya wengi. Tutajenga shule kusaidia Wakenya,” alisema.

• Omondi kupitia Sisi Kwa Sisi amekuwa akichangisha pesa kupitia ushawishi wake kubwa kwenye mtandao wa Instagram.

Mwanaharakati Eric Omondi
Mwanaharakati Eric Omondi
Image: Screengrab// YouTube (KOM)

Mchekeshaji aliyegeukia uanaharakati, Eric Omondi amefichua kuwa wakfu wa Sisi kwa Sisi umefanikiwa kuchangisha Zaidi ya shilingi milioni 72 kutoka kwa wahisani mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia Wakenya wenye mahitaji ainati.

Akizungumza kwenye runinga ya TV47, Omondi alisema kwamba alianzisha wakfu wa Sisi kwa Sisi kama njia moja ya kurudisha mkono kwa jamii, baada ya kuvuma kwenye tasnia ya uchekeshaji kwa Zaidi ya miaka 16.

Omondi alisema kuwa alianza kuwarai watu katika mitandao ya kijamii kujumuika naye kuchangisha chochote kidogo walicho nacho kuwasaidia wenzao miezi 7 iliyopita, na tayari ameshagusa nyoyo za watu 68 wenye mahitaji mbalimbali.

“Mpaka sasa tumesaidia watu 68, na tumechangisha Zaidi ya shilingi milioni 72 za Kenya katika kipindi cha miezi 7. Tutaendelea kuwasaidia Wakenya wa kila aina kwa sababu tunajua Wakenya wanajipambania wenyewe. Hatutalegeza Kamba, kusema kweli, ndio mwanzo tunaanza,” Omondi alimhakikishia Betty Kyallo.

Omondi alisema kwamba anakwenda kuweka mifumo ambayo itahakikisha mamilioni ya hela zinazochangishwa na Wakenya zitawasaidia mamilioni ya Wakenya, akisema kwamba kando na kusaidia mtu binafsi, atakwenda kuanzisha miradi ya kusaidia jamii nzima, kama mradi wa ujenzi wa daraja alioukamilisha katika kaunti ya Kisii miezi michache iliyopita.

“Tunaenda kuunda mfumo ambao utawezesha kusaidia Wakenya wengi. Tutajenga shule kusaidia Wakenya,” alisema.

Omondi kupitia Sisi Kwa Sisi amekuwa akichangisha pesa kupitia ushawishi wake kubwa kwenye mtandao wa Instagram.

Pesa hizo amekuwa akizitumia kuwasaidia Wakenya wenye mahitaji mbalimbali, haswa kipindi cha mafuriko ambayo yaliathiri mamia ya wakaazi wa mitaa duni jijini Nairobi.