Bahati na Diana Marua; familia ya kwanza Kenya kuwa na Reality Show kwenye Netflix!

“Tulikuwa Familia ya Kwanza ya Wakenya kuwa na Kipindi cha uhalisia kwenye Televisheni ya Kitaifa (Being Bahati kwenye NTV) na sasa tunaweka Historia kama Familia ya Kwanza ya Wakenya kuwa na Kipindi cha Uhalisia kwenye Netflix."

Muhtasari

•  Bahati alichapisha bango akifichua kwamba watazindua shoo hiyo ya uhalisia Alhamisi ya Juni 6 na itakuwa inakwenda kwa jina ‘The Bahati’s Empire’.

Bahati na Diana
Bahati na Diana

Wanandoa wa nguvu, Diana Marua na mumewe Kevin Bahati Kioko kwa mara nyingine wamedokeza kuweka historia ya kuwa wanandoa wa kwanza kutoka nchini Kenya kuwahi kufanya shoo ya uhalisia ambayo itapakiwa kwenye jukwaa kubwa Zaidi duniani la kupakua filamu la Netflix.

Kupitia kurasa zao mitandaoni, wanandoa hao ambao mwishoni mwa mwaka jana walisherehekea miaka 7 katika ndoa walifichua taarifa hizo, saa kadhaa baada ya kutaniani kwa jumbe za kuachana na kutupiana vijembe mitandaoni.

Bahati alichapisha bango akifichua kwamba watazindua shoo hiyo ya uhalisia Alhamisi ya Juni 6 na itakuwa inakwenda kwa jina ‘The Bahati’s Empire’.

“Tulikuwa Familia ya Kwanza ya Wakenya kuwa na Kipindi cha uhalisia kwenye Televisheni ya Kitaifa (Being Bahati kwenye NTV) na sasa tunaweka Historia kama Familia ya Kwanza ya Wakenya kuwa na Kipindi cha Uhalisia kwenye Netflix 🔥 Utukufu Wote Unamwendea Bwana Wetu Yesu Kristo,” Bahati alichapisha.

Msanii huyo ambaye si mgeni kwa jambo la kiki alijitapa kwamba wao ndio wanandoa wa kwanza si tu kutoka Kenya bali kutoka ukanda mzima wa Afrika Mashariki ambao watakuwa na kipindi cha uhalisia kwenye jukwaa la Netflix.

“Ni rasmi! Onyesho la kwanza la uhalisia wa kenya /east african kwenye netflix ni #thebahatisempire premiers on ijumaa tarehe 7 june 2024… Oh Ndiyo; I Know Y'all had Missed Us on TV… The King & Queen of Reality Wamerudi na Ni Wakati wa sisi kujibu Fununu zako zote tunaposhiriki na Ulimwengu Nyakati zetu Mchafu, Safi, Huzuni na Furaha! Hii haijaandikwa… huu ndio uhalisia bora kabisa imewahi kuona kenya… just trust me! Tazama kwenye netflix ijumaa hii,” aliongeza.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wamewaosoa vikali kutokana na mbinu waliyoitumia ili kutangaza ujio wa kipindi hicho cha uhalisia.

Wawili hao siku moja iliyopita walikiwasha kwenye mitandao ya kijamii baada ya kusitisha urafiki wao haswa kwenye mtandao wa Instagram kisha kuanza kuchapisha picha za kudhalilishana huku wakifuatisha emoji za kuvunjika moyo.