Bunny Asila kutoa msaada wa maji kwa waandamanaji wa Gen Z Nairobi na Nakuru

Msanii huyo mwenye makao yake nchini Ufini alisema tayari ametoa kreti 200 za maji ambayo yatasambazwa kwa waandamanaji katika miji ya Nakuru na Nairobi wakati watakapokuwa wakimenyana na vitoza machozi

Muhtasari

• Hata hivyo, msimamo wa vijana wengi ni kwamba mswada wote unafaa kutupiliwa mbali na si kufanyiwa marekebisho katika baadhi ya vipengele.

BUNNY ASILA
BUNNY ASILA
Image: FCEBOOK

Msanii namba moja wa injili ya Kenya barani Ulaya, Bunny Asila ameweka wazi msimamo wake kuhusu mswada tata wa fedha wa mwaka 2024.

Kupitia video aliyorekodi akitoa msimamo wake, Asila alisema kwamba ameungana na mamia ya vijana wa Gen Z ambao wanaupinga vikali mswada huo akisema kuwa baada ya kuupekua kwa umakini mkubwa, amekubaliana na vijana hao kwamba mswada huo ni wa kuwaumiza wananchi wa kawaida.

“Kuna hii stori ya mswada wa fedha 2024, nimechukua muda wangu na kuichambua na kuipekua. Mimi na jeshi langu tunaukataa. Kwa sababu hizo sera kwa kweli zinaumiza Mkenya wa kawaida,” Asila alisema.

Aidha, alikwenda mbele na kutoa ahadi ya kuonyesha kuwaunga mkono vijana waandamanaji kwa vitendo na wala si kwa maneno tu.

Asila ambaye alionesha nia yake ya kujiunga na vijana hao kwenye mitaa kushiriki maandamano alisema kwa bahati mbaya Jumanne hatokuwepo lakini akatoa ahadi ya kuwapa msaada wa maji.

Msanii huyo mwenye makao yake nchini Ufini alisema tayari ametoa kreti 200 za maji ambayo yatasambazwa kwa waandamanaji katika miji ya Nakuru na Nairobi wakati watakapokuwa wakimenyana na vitoza machozi wakati wa maandamano.

“Kwa hiyo Jumanne sitakuwa Nairobi, na kutokana na hilo, mimi na jeshi langu tumetoa maji kreti 200 Nairobi na Nakuru. Kama uko Nairobi au Nakuru wakati unafanya maandamano Jumanne, bajeti ya maji iko kwangu. Timu ya Bunny Asila itakuwa mitaani kusambaza maji, kwa hiyo wewe ukitembea ukifanya shughuli zako, mambo ya maji usikuwe na shaka,” alisema.

Kando na maji kwa waandamanaji wa Gen Z, Asila pia alisema timu yake itakuwa inatoa viburudisho vya kila aina kwa vijana hao katika miji hiyo miwili watakapokuwa wakiandamana kupinga kupitishwa kwa mswada tata wa fedha 2024.

“Refreshments zote ni kwa Bunny Asila, hebu sote tukatae mswada wa fedha wa 2024, ahsante,” alisema.

Vijana wa Gen Z walianza maandamano yao wiki jana kwa kuyaratibu kupitia mitandao ya kijamii na baadae kujitokeza kwa wingi katika miji mbali mbali wakiwa wamejihami kwa simu zao za mkononi, maji, vitambaa na akili zao bila silaha yoyote.

Waliandamana Jumanne na Alhamisi wakilalamika kupitishwa kwa mswada huo ambao ulipigiwa kura ya kuukubali na wabunge 204 huku wabunge 115 wakipiga kura ya kuukataa.

Vijana hao aidha wametangaza kufanyika kwa maandamano Zaidi Jumanne wiki hii wakati mswada huo utakapofikishwa bungeni kufanyiwa marekebisho ili kuondoa vupengele vilivyokataliwa.

Hata hivyo, msimamo wa vijana wengi ni kwamba mswada wote unafaa kutupiliwa mbali na si kufanyiwa marekebisho katika baadhi ya vipengele.