Eric Omondi aeleza kwa nini ameamua kuondoka Nairobi na kurudi Siaya kijijini

“Unajua sahi ndio ukweli unanigonga kwamba tumepoteza Fred, sahi ndio inani’hit. Sasa hivi ni kama niko in denial, niko in shock. Na hivyo naona kama inanilemea na ndio maana sitaki kukaa Nairobi."

Muhtasari

•  Wki jana, kamati ya mipangilio ya mazishi hayo ilitoa ratiba kwamba Fred atazikwa Jumamosi ya mwisho wa mwezi Juni baada ya kuhusika katika ajali wiki mbili zilizopita jijini Nairobi.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: Screengrab//Trudy Kitui YT

Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi amefichua kwamba ameamua kurudi kijijini kwao Sega kaunti ya Siaya hii wiki wakati ambapo maandalizi ya mazishi ya mdogo wake, Fred Omondi yanaendelea kuratibiwa.

 Wki jana, kamati ya mipangilio ya mazishi hayo ilitoa ratiba kwamba Fred atazikwa Jumamosi ya mwisho wa mwezi Juni baada ya kuhusika katika ajali wiki mbili zilizopita jijini Nairobi.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani wikendi iliyopita baada ya kukamilika kwa hafla ya Last Laugh kwa ajili ya Fred, iliyoandaliwa na wachekeshaji wenza katika ukumbi wa Carnivore jijini Nairobi, Eric alisema kwamba ameamua kurudi nyumbani ili kujituliza kiasi.

Omondi alisema kwamba mwanzoni haikuwa imemuingia kuamini kwamba mdogo wake amefariki lakini sasa ndio ukweli umeanza kumpiga makofi usoni na ameamua kurudi kijijini kama njia moja ya kupata therapy.

“Hii wiki itakuwa ngumu kwa kweli, niko na fatigue lakini tutapitia tu. Angalau kamati imesimamia mambo mengi kwa sasa, mimi naenda kijijini leo. Unajua ushagoo kuna miti, kuna mito… ni kama therapy, lakini imekuwa ngumu sana katika kipindi cha wiki moja iliyopita,” Eric alisema.

“Unajua sahi ndio ukweli unanigonga kwamba tumepoteza Fred, sahi ndio inani’hit. Terence aliniambia nitalia, sasa hivi ni kama niko in denial, niko in shock. Na hivyo naona kama inanilemea na ndio maana sitaki kukaa Nairobi. Nimeona tu niende nyumbani nikae huko, nitarudi tena wakati wa ibada ya wafu tukichukua mwili,” aliongeza.

Kuhusu jinsi alipokea taarifa za kifo cha mdogo wake, Eric aliyeonekana mwenye mawazo mengi sana alisema;

“Habari za kifo cha Fred zilinigonga vibaya sana, Terence alinipigia simu, kwa hivyo hii siku simu yangu ilikuwa imezima, Lynne aliniamsha alfajiri ya 6am akisema Terence anataka nimpigie simu mara moja. Nilipompigia aliniambia nikimbie Mama Lucy kuona Fred amepata ajali. Vile nilisikia ni ajali ya Pikipiki, nilichanganyikiwa sana sababu najua ajali za pikipiki huwa mbaya.”