Churchill atangaza tarehe kamili kipindi chake cha uchekeshaji kitarejea hewani NTV

Muhimu Zaidi, Churchill aliweka wazi msimamo wake kuhusu sakata zima linalopandisha joto la kisiasa humu nchini kuhusu maandamano na Gen Z kupinga muswada wa kifedha wa 2024.

Muhtasari

• Muhimu Zaidi, Churchill aliweka wazi msimamo wake kuhusu sakata zima linalopandisha joto la kisiasa humu nchini kuhusu maandamano na Gen Z kupinga muswada wa kifedha wa 2024.

Mchekeshaji Daniel Ndambuki maarufu kama Churchill amefichua tarehe kamili kipindi cha Churchill Show kitarejea hewani NTV.

Churchill Show ambayo kwa mara ya kwanza ilikwenda hewani NTV mwaka 2007 waliondoka mwezi Mei 2022 na baada ya miaka miwili, Jumatatu walitangaza kurejea walipoanzia, NTV.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani baada ya kusaini mkataba mpya na NTV, Churchill alifichua kwamba kipindi hicho cha uchekeshaji ambacho kiliwatoa wachekeshaji wengi kitarejea kwa mara ya kwanza Julai hii.

“Shoo inaanza tarehe 13 mwezi Julai kuanzia saa mbili usiku,” Churchill alisema.

Kuhusu wazo la kuamua kurudi NTV baada ya kuhamia TV 47 kwa kipindi kifupi kisha kuingia gizani, Churchill alisema;

“Tumerudi tena mahali kila kitu kilianzia miaka mingi iliyopita. Ni watu wameitisha kipindi kirejee kwa sababu tunapitia mambo mengi sana kama nchi na ni vizuri watu waondoe stress kiasi kwa vichekesho. Watu ndio wamerewuest, wakitutumia barua pepe na kutupigia simu pia hadi kupiga simu NTV, haya basi tumeamua kuwarejeshea kipindi chenu, sisi ni washikadau, sisi ni kushikilia tu,” Churchill alisema.

Muhimu Zaidi, Churchill aliweka wazi msimamo wake kuhusu sakata zima linalopandisha joto la kisiasa humu nchini kuhusu maandamano na Gen Z kupinga muswada wa kifedha wa 2024.

“Najua rais amesema tutaenda kuwa na mazungumzo, hilo ni jambo ambalo lingefanyika kitambo sana, kwa hiyo wacha watu wajieleza jinsi wanahisi. Huwezi kuwa uko peke yako pale na wengine wanaelekea huku, kila mtu hawezi kuwa amekosea, lazima tusimame pamoja, kama kuna kasoro kuna kasoro, hivyo pia mimi nina’reject huo muswada wa fedha,” Churchill alisema.