“Sijawahi kufaidika na kitu chochote kutoka kwa serikali ya Ruto!” – Millicent Omanga

“Nahitaji kufuta dhana potofu. Mimi Millicent Omanga sifanyi kazi kwa serikali ya Kenya wala sina zabuni yoyote katika serikali hii. Mimi ni mtu binafsi ninafanya biashara binafsi" Omanga alisema.

Muhtasari

• Baadhi walikuwa wanadai kwamba amekuwa akipata zabuni za serikali katika kusambaza bidhaa mbali mbali, jambo ambalo Omanga alikanusha wazi wazi.

MILLICENT OMANGA NA RAIS WILLIAM RUTO
MILLICENT OMANGA NA RAIS WILLIAM RUTO
Image: FACEBOOK

Aliyekuwa mgombea wa uwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nairobi, Millicent Omanga ameweka wazi kwamba vitu vya thamani ambavyo amekuwa akivionyesha kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni havina uhusiano wowote na serikali hii ya Kenya Kwanza.

Omanga alilazimika kujibu kuhusu mali yake na haswa gari jipya aina ya Range Rover ambalo alilionesha mitandaoni siku chache zilizopita kabla ya maandamano ya Gen Z kung’oa nanga.

Baadhi walikuwa wanadai kwamba amekuwa akipata zabuni za serikali katika kusambaza bidhaa mbali mbali, jambo ambalo Omanga alikanusha wazi wazi.

Omanga, ambaye aliwahi kuwa mbunge maalum katika bunge liilopita alitupilia mbali madai kwamba amekuwa akifaidika kutoka kwa serikali ya Ruto ambayo amekuwa akiitetea juu chini.

Hata hivyo, alinyoosha maelezo yake kwamba hajawahi kufaidika kwa njia yoyote kutoka kwa serikali ya Ruto, akiweka wazi kuwa hapokei mshahara wowote licha ya kuteuliwa kama msaidizi wa waziri katika wizara ya usalama wa ndani, nyadhifa ambazo hata hivyo zilitupiliwa mbali na mahakama mwaka jana.

“Nahitaji kufuta dhana potofu. Mimi Millicent Omanga sifanyi kazi kwa serikali ya Kenya wala sina zabuni yoyote katika serikali hii. Mimi ni mtu binafsi ninafanya biashara binafsi. Isitoshe, sijawahi kufaidika na serikali hii iwe kwa pesa taslimu au kwa hisani. Nilitaka kuweka hili wazi!” Omanga alisema huku akitoa nafasi kwa watu kumuuliza maswali yoyote.