Anjella amsuta Mwijaku kwa kutaka Diamond kumshukuru Harmonize kabla ya kumpa shoo

Diamond na Nandy, walimualika Anjella kutumbuiza katika matamasha ya Wasafi Festival na Nandy Festival, jambo ambalo Mwijaku alisema wanafaa kumshukuru kwanza Harmonize kwa kumleta Anjella kwenye mwanga.

Muhtasari

• "Siku nyingine kabla ya kuandika nifikirie mimi, wafikirie na unaowalenga. Mimi ndiye ninayetakiwa kuvuka mto ila wewe kaka yangu umenitukania mamba,” Anjella alimaliza.

ANJELLA AMSUTA MWIJAKU KUTAKA NANDY NA DIAMOND KUMSHUKURU HARMONIZE
ANJELLA AMSUTA MWIJAKU KUTAKA NANDY NA DIAMOND KUMSHUKURU HARMONIZE
Image: INSTAGRAM

Aliyekuwa msanii wa lebo ya Konde Music Worldwide, Anjella amsuta vikali mtangazaji Mwijaku baada ya mtangazaji huyo kudai Diamond na Nandy wanamtumia Anjella kuendelea kuvuma mjini.

Diamond na Nandy, walimualika Anjella kutumbuiza katika matamasha ya Wasafi Festival na Nandy Festival, jambo ambalo Mwijaku alisema wanafaa kumshukuru kwanza Harmonize kwa kumleta Anjella kwenye mwanga.

Akimjibu, Anjella alisema kwamba anachokifanya Mwijaku ni kama kumharibia riziki yake mjini kwani kwa kuwataka watu kumshukuru Harmonize kabla ya kumpa Anjella shoo yoyote kutafanya watu wengi kumkwepa mrembo huyo katika kumpa shoo.

Anjella alifafanua hata hivyo kwamba anaheshimu kwa kiasi kikubwa mchango wa Harmonize kwake lakini hilo lisimfanye kuwakumbusha kila mtu anayetaka kumsaidia, kwani tayari ukurasa wa Konde Gang umeshafungwa kwake na sasa ni yeye kujitafuta upya.

“Kaka yangu Mwijaku, ninaheshimu sana mchango wa Harmonize katika taaluma yangu ya muziki. Lakini unaposema kwamba hizi festival mbili ambazo nimealikwa ni tobo kwao, huoni kama utanikosesha riziki?” Anjella alimuuliza Mwijaku.

“Kumnbuka wao ni wakubwa kuniliko mimi na hata nisipokuwepo hawapungukiwi kitu kwa sababu wasanii tupo wengi. Siku nyingine kabla ya kuandika nifikirie mimi, wafikirie na unaowalenga. Mimi ndiye ninayetakiwa kuvuka mto ila wewe kaka yangu umenitukania mamba,” Anjella alimaliza.