"Ananifanya nijisikie mtoto mdogo!" Akothee asifia mahaba ya mpenziwe mzungu

Akothee alibainisha kuwa mpenziwe alichagua kuwa pale kwa ajili yake.

Muhtasari

• Bw Omondi aliandamana na malkia huyo wake kwenye hafla ya Pwani Golden Awards  ambayo iliandaliwa jijini Mombasa.

•Walionekana wameshikana mikono huku wakitembea kwenye hafla hiyo ambayo  ilihudhuriwa na wasanii mbalimbali wa Kenya.

Akothee na mpenzi wake Omosh
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na Mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee ameendelea kujigamba kuhusu mahaba Ndi Ndi Ndi anayomiminiwa na mchumba wake mzungu ambaye amebatiza jina Bw Omondi.

Wikendi, Bw Omondi aliandamana na malkia huyo wake kwenye hafla ya Pwani Golden Awards  ambayo iliandaliwa jijini Mombasa. Akothee alibainisha kuwa mpenziwe huyo kijana alichagua kuwa pale kwa ajili yake.

"Eish, anafanya nijiskie mchanga. Alisema, nitakulinda, nitakuwa hapo kwa ajili yako, ninajivunia wewe mke wangu," Akothee aliandika chini ya picha zake na mpenziwe ambazo alichapisha kwenye Facebook.

Aliendelea kujitambulisha yeye na mchumba wake kama Bw na Bi Omosh. Pichani, wapenzi hao walionekana wameshikana mikono huku wakitembea kwenye hafla hiyo ambayo  ilihudhuriwa na wasanii mbalimbali wa Kenya.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye alikuwa amealikwa kutumbuiza katika hafla hiyo ya siku ya Jumamosi pia alijivunia jinsi waandishi wa habari walivyotaka sana kumhoji yeye na mpenzi wake.

Siku chache kabla ya hafla hiyo, Bw Omosh alimpeleka mchumba huyo wake hospitalini baada ya kukumbwa na maumivu ya kichwa kwa siku kadhaa.

"Tumekuwa na siku tano mbaya za maumivu makali ya kichwa , muda mwingi jana tulikaa hospitalini, Omondi aliogopa sana kunipeleka katika hospitali yoyote hapa kijijini, safari zote za ndege kutoka kisumu hadi Mombasa zilikuwa zimebookiwa kabisa," alisema siku ya Ijumaa, wiki iliyopita.

Akothee alibainisha kuwa hakuna ugonjwa wowote ambao uligunduliwa baada ya kufanyiwa vipimo. Alidokeza kuwa masaibu yaliyomkumba yanahusishwa na uchovu na hivyo kutangaza atachukua muda wa mapumziko.

"Hivyo ina maana Punda Amechoka tu. Ni mapumziko ya kitandani tena," alisema.

Mama huyo wa watoto watano alimsifia mpenziwe kwa hatua ya kumshughulikia na akawashauri wanawake wasio na waume kuolewa.

Aliwabainishia wanawake kwamba kuwa na mwanaume kando yao ni jambo zuri kwani wanaweza kuwa msaada mkubwa kwao katika nyakati ngumu.

"Akina mama single, ili kutulia, mbadilishe Mr Wrong  umfanye awe mzuri. Nani atakupeleka hospitali na utaliban wako huo wa Miss Independent. My dear, heshimu ndoa,"alisema.

Akothee alimtambulisha Omosh kama mpenziwe mpya mnamo mwezi Septemba, miezi kadhaa baada ya kutengana na Nelly Oaks.