Akothee apelekwa hospitalini na mpenziwe baada ya kuugua, awahimiza wanawake waolewe

Mwimbaji huyo alimhakikishia mpenzi wake kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Muhtasari

•Akothee aliwabainishia wanawake kwamba kuwa na mwanaume kando yao ni jambo zuri kwani wanaweza kuwa msaada mkubwa katika nyakati ngumu.

•Alidokeza kuwa masaibu yaliyomkumba yanahusishwa na uchovu na hivyo kutangaza atachukua muda wa mapumziko.

Image: FACEBOOK// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akothee almaarufu Akothee amewahimiza akina mama wasio na waume kuolewa.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watano aliwabainishia wanawake kwamba kuwa na mwanaume kando yao ni jambo zuri kwani wanaweza kuwa msaada mkubwa katika nyakati ngumu.

"Akina mama single, ili kutulia, mbadilishe Mr Wrong  umfanye awe mzuri. Nani atakupeleka hospitali na utaliban wako huo wa Miss Independent. My dear, heshimu ndoa," Akothee alisema siku ya Ijumaa.

Matamshi hayo yake yalikuja baada ya mpenzi wake mzungu Bw Omosh kumpeleka hospitalini siku ya Alhamisi baada ya kuumwa na kichwa mara kwa mara katika kipindi cha takriban wiki moja iliyopita.

"Tumekuwa na siku tano mbaya za maumivu makali ya kichwa , muda mwingi jana tulikaa hospitalini, Omondi aliogopa sana kunipeleka katika hospitali yoyote hapa kijijini, safari zote za ndege kutoka kisumu hadi Mombasa zilikuwa zimebookiwa kabisa," alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 alibainisha kuwa hakuna ugonjwa wowote ambao uligunduliwa baada ya kufanyiwa vipimo. Alidokeza kuwa masaibu yaliyomkumba yanahusishwa na uchovu na hivyo kutangaza atachukua muda wa mapumziko.

"Hivyo ina maana Punda Amechoka tu. Ni mapumziko ya kitandani tena," alisema.

Aidha alimhakikishia mpenzi wake kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mjasiriamali huyo kuchukua mapumziko ya siku tano kutokana na uchovu.

Mapema mwezi uliopita alilalamika kuwa anahisi kuchoka sana, jambo ambalo lilimlazimu kupumzika kwa siku chache.

"Nimekuwa nikifanya mengi na ninahisi uchovu, kwa hivyo kwa upole nitakuwa na mapumziko ya kitandani ya lazima ya siku tano," alisema.

Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa hangepokea simu katika kipindi hicho cha mapumziko na pia akaomba asiitwe kwa mikutano yoyote.

Alieleza kwamba alichoka akizunguka zunguka kukusanya vifaa vya ujenzi wa shule yake ya, Akothee Foundation Academy.

"Leo nimefanya na nimemaliza. Acheni nichukue mapumziko ya siku tano. Nitarudi. Nawapenda," alisema.

Akothee aliendelea kuchukua mapumziko kama alivyotangazwa na alikosekana mitandaoni kwa takriban wiki moja.