"Asante Hakimi!" Lofty Matambo adokeza kuandikisha mali chini ya jina la mamake

Mtangazaji wa habari Lofty Matambo alishiriki muda na chakula kizuri na mamake katika hoteli moja Kilifi.

Muhtasari

•Matambo na mamake walionekana wenye furaha huku wakishiriki chakula cha mchana pamoja katika mkahawa wa Vipingo Ridge.

•Matambo alidokeza kwamba mazungumzo yao huenda yalihusisha jinsi angeweka mali yake chini ya jina la mzazi huyo.

wakishiriki chakula katika Vipingo Ridge.
Lofty Matambo na mama yake wakishiriki chakula katika Vipingo Ridge.
Image: FACEBOOK// LOFTY MATAMBO

Siku ya Jumanne, mwanahabari mashuhuri Lofty Matambo alichapisha picha yake nzuri akiwa na mama yake mzazi.

Matambo alikuwa amemtembelea mzazi huyo wake katika kaunti ya nyumbani kwao Kilifi na pichani walionekana wenye furaha tele huku wakishiriki chakula cha mchana pamoja katika mkahawa wa Vipingo Ridge.

"Niko hapa na Mamangu, unaweza kukisia mazungumzo yanahusu nini," alisema kwenye sehemu ya maelezo ya picha hiyo.

Mtangazaji huyo wa habari mwenye uzoefu mkubwa hasa kwa matangazo ya lugha ya Kiswahili aliendelea kudokeza kwamba mazungumzo hayo huenda yalihusisha jinsi angeweka mali yake chini ya jina la mzazi huyo.

Alimshukuru beki wa PSG Achraf Hakimi kwa kile kinachoweza kuwa, kumtia msukumo wa kumpa mamake heshima hiyo.

"Asante Hakimi," alisema.

Mamia ya watumiaji wa Facebook walikuwa wepesi kumpongeza mtangazaji huyo wa habari kwa kumthamini mzazi huyo wake.

Mtangazaji Lofty Matambo alizaliwa na kukulia katika kaunti ya Kilifi, eneo la Pwani kabla ya kuhamia jijini Nairobi miaka kadhaa iliyopita kwa ajili ya kazi. Mwanahabari huyo anafahamika zaidi kwa weledi wake katika matangazo, mahojiano na mazungumzo ya lugha ya Kiswahili kwenye runinga.

Mchezaji wa timu ya taifa ya Morocco Achraf Hakimi, ambaye alitajwa na Matambo, amekuwa akivuma siku za hivi majuzi kufuatia madai kuwa ameandikisha mali na utajiri wake wote chini ya mama yake mzazi.

Hakimi alisemekana kuandikisha mali yake yote kwa jina la mama yake, Bi Saida Mouh, wakati aliyekuwa mke wake, Hiba Abouk alipochukua kesi ya kutaka talaka akidai kupewa zaidi ya nusu ya mali ya mumewe.

Kwa mshangao mkubwa, mahakama ilidaiwa kubainisha kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 hakuwa na mali hata kidogo, urithi wake mwingi ukiwa chini ya miliki ya mama yake mzazi.

Mtandaoni, makundi yamekuwa yakihasimiana kufuatia uamuzi wa Hakimi kumpa mama yake mali yake, wavulana wakifurahi na kusema kuwa mchezaji huyo ndiye himizo lao huku kina dada wakionekana kusimama upande wa Bi Abouk wakisema Hakimi hakumfanyia vizuri ikizingatiwa wana watoto wawili pamoja.