Alichokisema Nyamu baada ya Eliud Kipchoge kudhalilika kwenye mbio za Boston

Nyamu kama Wakenya wengine tu alijiuliza ni nini kilimkuta Kipchoge mpaka kutupwa hadi nafasi ya sita mbali na mshindi wa mbio hizo Chebet.

Muhtasari

• Kulingana na Nyamu, ni wakati sasa Kipchoge astaafu ili kulisitiri jina lake la heshima kwani kuendelea kushiriki na kushindwa na kujidhalilisha zaidi.

Karen Nyamu atoa maoni yake baada ya Kipchoge kushindwa katika mbio za Boston.
Karen Nyamu atoa maoni yake baada ya Kipchoge kushindwa katika mbio za Boston.
Image: Instagram (Nyamu) , Facebook (Kipchoge)

Seneta mteule Karen Nyamu amedokeza maoni yake kuhusu kushindwa kwa mshikilizi wa rekodi Eliud Kipchoge katika mbio za Boston Marathon.

Mwanariadha mashuhuri wa Kenya alimaliza wa sita katika mbio hizo, akitumia muda wa 2:09:23 katika mbio alizoshinda mzalendo Evans Chebet aliyetumia dakika 2:05:54.

Kwa hivyo Chebet anakuwa mwanariadha wa kwanza wa kiume kuhifadhi taji lake katika mbio hizo hizo.

Nyamu kama tu Wakenya wengine alishangaa ni nini kimemkuta gwiji wa mbio za masafa marefu Eliud Kipchoge ambaye katika mbio za hivi karibuni amekuwa akishindwa tena kwa kumaliza nafasi zisizofurahisha wala kutoa taswira kamili ya yule Kipchoge ambaye wengi walimzoea kwa weledi kwenye mbio hizo.

“Imekuwaje kwaGOAT wetu? Je, ni wakati wa kutoka jukwaani na kupata urithi usioshuhudia siku mbaya zaidi mbeleni?" aliuliza Nyamu.

Katika maoni yake baada ya kinyang'anyiro hicho, Kipchoge, 38, alikubali kushindwa, akiongeza kuwa anatazamia kuimarika katika mbio zinazofuata.

"Ninaishi kwa wakati ambapo ninaweza kupinga mipaka. Haijahakikishiwa kamwe, na sio rahisi kamwe. Leo ilikuwa siku ngumu kwangu. Nilijikakamua kadiri nilivyoweza lakini wakati mwingine, lazima tukubali kwamba leo haikuwa siku ya kusukuma kizuizi kwa urefu zaidi," Kipchoge alisema.

Mnamo 2020, Kipchoge alimaliza wa nane katika mbio za London Marathon kwa saa 2:06:49, zaidi ya dakika moja nyuma ya mshindi Shura Kitata wa Ethiopia.

Anatarajiwa kukimbia marathoni mbili zaidi kabla ya Michezo ya Paris. Kipchoge atakuwa karibu miaka 40 kuelekea mbio za Paris, zaidi ya mwaka mmoja zaidi ya bingwa mkongwe zaidi wa Olimpiki katika mashindano yoyote ya mbio, kulingana na Olympedia.org. Kenya bado haijataja timu yake ya wachezaji watatu wa mbio za marathon za Olimpiki.