Eric Omondi afunguka jinsi Moses Kuria alivyomsaidia wakati matatizo yalipomkumba

Mchekeshaji huyo amesema kuwa Kuria amefanya mengi mazuri ambayo yanastahili kutuzwa.

Muhtasari

• Eric amesema kuwa aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria anastahili wadhifa wa uwaziri aliokabidhiwa mapema wiki hii.

•Pia amesema kuwa Kuria amewasaidia vijana wengi kukuza talanta zao za sanaa kupitia stesheni yake ya runinga.

Eric Omondi, Moses Kuria
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi amesema kuwa aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria anastahili wadhifa wa uwaziri aliokabidhiwa mapema wiki hii.

Siku ya Jumanne rais William Ruto alimteua kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi kuwa waziri mpya wa Biashara na Viwanda.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Eric Omondi amesema kuwa Kuria amefanya mengi mazuri ambayo yanastahili kutuzwa.

"Moses amekuwa akinisaidia pamoja na kundi lingine la vijana kwa miaka mingi. Nakumbuka miaka 8 iliyopita alipofadhili ziara yetu ya kwanza ya Marekani na @chipukeezy hadi New York, Dalas na baadaye Kujiunga nasi Vegas siku ya Ukumbusho wa onyesho letu," mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama aliandika.

Eric pia alifichua kuwa mbunge huyo wa zamani alimsaidia sana na kusimama naye kipindi ambapo hatua yake ya kufungua ofisi na kampuni ya sanaa ya Big Tyme Productions ilipingwa na zikataka kufungwa.

Pia amesema kuwa Kuria amewasaidia vijana wengi kukuza talanta zao za sanaa kupitia stesheni yake ya runinga.

"Akiwa na Fanaka TV alisaidia vijana wengi kupitia ajira na Mafunzo ya Ufundi, hili nililishuhudia," Eric amesema.

Mchekeshaji huyo ameeleza imani yake kuwa Kuria atafanya kazi katika wizara ya Biashara na Viwanda aliyokabidhiwa.

"Amegusa msingi na Vijana Wajasiriamali wa Taifa hili na anaelewa jukumu kikamilifu. Asante mtukufu Rais wako na HONGERA SANA MHESH!!!," alisema

Kabla ya kuteuliwa kuwa waziri Kuria aliwania kiti cha ugavana wa Kiambu katika kinyang'anyiro cha Agosti 9.

Hata hivyo hakuweza kunyakua kiti hicho na akakubali kushindwa na Kimani Wamatangi wa UDA hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa.