King Kaka afunguka jinsi alivyopona kimiujiza baada ya kuugua kupata ufunuo wa ajabu

Aliruhusiwa kuenda nyumbani siku tano baada kupata ufunuo wa ajabu usiku.

Muhtasari

•King Kaka alifichua kuwa alipiga hatua ya kuenda hospitali baada ya ugonjwa kumlemea zaidi hadi kiwango alihisi kama angekufa.

•Alisema baada ya kufichuliwa mambo ya ajabu alimuomba Mungu na kufanya amani naye kwani alihisi anakaribia kufa.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu King Kaka amebainisha kuwa yeye kuwa hai na kuweza kufanya mambo kadhaa ya kawaida kama vile kula na kutembea ni muujiza.

Mwishoni mwa mwaka wa 2021, King Kaka aliugua sana baada ya kufanyiwa vipimo vya afya vibaya. Alipoteza zaidi ya kilo 30 katika kipindi cha miezi minne ambacho alikuwa alikuwa akipambana na ugonjwa usiotambuliwa.

Katika mahojiano na Oga Obinna kwenye Kula Cooler Show, mwanamuziki huyo alifichua kuwa alipiga hatua ya kuenda hospitali baada ya ugonjwa kumlemea zaidi hadi kiwango alihisi kama angekufa.

"Siku moja mke wangu alitoka kazini nikamwambia naona kama nitatolewa hapo ndani ya mfuko wa kubebea mwili na sitaki watoto waone hilo. Nilimwambia tuchague hospitali yoyote ile nitalala huko," alisimulia.

Alisema baada ya kufika hospitali alilazwa na madaktari wakaanza kumfanyia vipimo kadhaa bila kupata ugonjwa wowote. Miongoni mwa magonjwa aliyopimwa ni TB, UKIMWI, Saratani miongoni mwa mengine.

"Ilifika wakati nilikuwa naomba ugonjwa," alisema.

King Kaka alifichua kwamba mchakato wa uponyaji wake ulianza usiku mmoja wakati bado akiwa amelazwa katika hospitali ambapo alianza kuona mambo yasiyo ya kawaida mwendo wa saa tisa usiku.

"Nilianza kuona vitu sijui. Nilianza kuona mwangaza, nikaona giza. Niliona ni wakati wangu wa kuishia. Niliambia Mungu kama wakati wangu niko tayari. Huwa inafika mahali hata unakubali kifo," alisimulia.

Alisema baada ya kufichuliwa mambo ya ajabu alimuomba Mungu na kufanya amani naye kwani alihisi anakaribia kufa.

Kiajabu, asubuhi iliyofuata alipata kifungua kinywa kwa mara ya kwanza baada ya siku tano hivi. Pia alikunywa supu baadaye.

"Hivyo ndivyo nilianza kula. Baada ya siku tatu, nne hivi nilikuwa natembea huko hospitali," alisema

Aliruhusiwa kuenda nyumbani siku tano baada kupata ufunuo wa ajabu usiku.