Massawe Japanni afawidhi hafla ya kuapishwa kwa Sakaja

Sakaja aliapishwa kama gavana wa 4 wa nairobi katika ukumbi wa KICC.

Muhtasari

• Japanni pia mwaka jana alisherehesha hafla ya Madaraka Juni mosi iliyohudhuriwa na mkuu wa majeshi rais Kenyatta na viongozi wengine.

Alikuwa mshereheshaji mkuu katika hafla ya kuapishwa kwa gavana Sakaja
Massawe Japanni Alikuwa mshereheshaji mkuu katika hafla ya kuapishwa kwa gavana Sakaja
Image: Instagram

Mtangazaji wa zamu ya mchana katika stesheni ya Radio Jambo Massawe Japanni ni mtu mwenye furaha baada ya kuwa mfawidhi mkuu katika hafla ya kuapishwa kwa gavana mteule wa Nairobi, Johnson Sakaja.

Akidhihirisha furaha yake kwenye mitandao yake ya kijamii, Japanni alipakia picha ya pamoja na mshereheshaji mwenza mtangazaji Jimmy Gathu na kusema kwamba ilikuwa moja ya siku yake ya furaha kusherehesha katika hafla hiyo kubwa ya kihistoria ya kaunti ya Nairobi kuapisha gavana wa nne, miaka 10 tangu ugatuzi.

“Washereheshaji waliofurahisha kuapishwa kwa Gavana Sakaja! Ni heshima iliyoje! @jsakaja Na gwiji @jimmigathu,” Japanni aliandika kwenye Istagram.

Sakaja aliyeshinda uchaguzi huo kupitia tikiti ya chama cha naibu rais anayeondoka William Ruto, UDA aliapishwa katika ukumbi wa KICC  ambapo Mamia ya wageni waalikwa wakiwemo wanasiasa mashuhuri walishuhudia kuapishwa kwa Sakaja mubashara. 

Kiongozi wa chama, Rais mteule William Ruto ni miongoni mwa wageni waliokuwa wamehudhuria.

Sakaja aliwasili katika ukumbi huo mwendo wa saa nne unusu asubuhi akiwa ameandamana na familia yake, wanawe wa kiume wawili na binti mmoja waliokuwa wamevalia nadhifu kweli kweli.

Hii si mara ya kwanza kwa mtangazaji huyo mwenye wepesi katika lugha ya Kiswahili kusherehesha kweney hafla za kihistoria kwani mwaka jana alikuwa mshereheshaji mkuu katika hafla ya kiserikali ya Madaraka ambayo huadhimishwa Juni mosi kila mwaka kusherehekea Kenya kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Katika hafla hiyo ya mwaka jana iliyoandaliwa kwenye bustani ya Uhuru Gardens, Lang’ata jijini Nairobi, Japanni walishirikiana na mtangazaji mwenza Mzazi Willy Tuva kulipakua tafrija hiyo iliyohudhuriwa na mkuu wa majeshi rais Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wengi.

Mke wake Beatrice Sakaja, wanawe wawili waliongozana naye kwenye hafla hiyo. Binti aliyekuwa pamoja nao sio wake.