(+video) "Nilifuatwa na wanasiasa niwafanyie ngoma za kampeni nikakataa" - Mejja

Nilihisi hata nitagawa watu zaidi - Mejja

Muhtasari

• "Hata nilipigia meneja simu juu walinisumbua sana hata waliendelea kusumbua kwa kurudi na kiasi kikubwa cha pesa kila mara nilipokataa,” Mejja alisema.

• Haya yanakuja siku chache tu baada ya watu kutoa maoni kwa nini wasanii wa Kenya hawataki kujihusisha na mirengo ya kisiasa.

Huku joto la ghadhabu kuhusu wasanii wan je ya nchi kutumbuiza katika mikutano ya kisiasa nchini Kenya likiendelea kutokota, Msanii Mejja sasa ameibuka na madai kwamba kwa wakati mmoja aliwahi tafutwa na baadhi ya wanasiasa wakimtaka kuwatungia ngoma ya kisiasa ila akakataa licha ya kuahidiwa kitika kikubwa cha pesa.

Katika mahojiano ya kipekee na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo swiki chache zilizopita, Mejja alisema kwamba licha ya dili hiyo kuwa nono, lakini bado aliikataa kwa kile alisema kwamab hakutaka kugawanya mashabiki wake kwa misingi ya mirengo ya kisiasa humu nchini.

“Nilifuatwa lakini sikuchukua. Nilihisi hata nitagawa watu zaidi. Niliona hata si kusaidia. Nilihisi nitakuwa sehemu ya kugawanya watu. Ilikuwa ngumu unajua mimi ni binadamu pia. Hata nilipigia meneja simu juu walinisumbua sana hata waliendelea kusumbua kwa kurudi na kiasi kikubwa cha pesa kila mara nilipokataa,” Mejja alisema.

Hii inakuja baada ya watu mbali mbali wakitoa maoni yao kuhusu wasanii wan je kupewa nafasi kubwa ya kutumbuiza humu nchini huku wasanii wa ndani wakizidi kukandamizwa kwa kunyimwa nafasi za kuonesha uwezo wao katika hafla kubwa kama hizo.

Mchekeshaji Eric Omondi aliwalaumu wasanii kwa kutojijenga vizuri ili kuwavutia wanasiasa kutaka kuwahitaji kwenye mikutano yao na kuwataka kuunga mkono kikamilifu mswada ambao aliuwasilisha bungeni kutaka muziki wa Kenya kupewa asilimia 75 ya miziki inayochezwa hewani.

Kwingineko mchekeshaji Alex Mathenge alisema wasanii wa humu nchini wanaogopa kushiriki katika mikutano ya kisiasa na kuonekana hadharani wakitumbuiza kwa kile alisema kwamab wasanii wengi wanategemea dili za ubalozi wa mauzo katika biashara za makampuni mbalimbali na pindi tu wanapoonekana kwenye mikutano ya kisiasa basi wanahatarisha kupokonywa dili hizo na kurudi katika umaskini mkubwa, kitu ambacho kila mtu anakipiga vita usiku na mchana.