"Wasanii tunaogopa kushiriki hafla za siasa juu tutapoteza dili za ubalozi wa mauzo" - Alex Mathenge

Jumamosi Wakenya walichukizwa na kitendo cha Diamond kutumbuiza kwenye hafla ya Azimio Kasarani.

Muhtasari

• "Utatumbuiza pale na kupoteza dili zote za kibiashara kuanzia,” alisema Mathenge.

 

Mchekeshaji Alex Mathenge akitilia neno lake katika wasanii na siasa za kenya
Mchekeshaji Alex Mathenge akitilia neno lake katika wasanii na siasa za kenya
Image: Instagram//Alex Mathenge

Wikendi iliyopita kulikuwepo na matukio mbalimbali jijini Nairobi, makubwa yakiwa yale ya mikutano ya mwisho ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Katika mikutano hiyo, mmoja ukiwa ule wa Kenya Kwanza ugani Nyayo na mwingine ukiwa ule wa Azimio ugani Kasarani, kote kulikuwepo na burudani ya kukata na shoka kutoka kwa wasanii mbalimbali.

Lililozua mjadala mkali mitandaoni ni kwamba katika hafla hizo zote, wasanii waliotumbuiza kileleni kabisa walikuwa kutoka nje ya Kenya, Diamond Platnumz kutoka Tanzania akifunika kabisa uwanja wa Kasarani naye msanii wa injili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Solomon Mkubwa akitamba katika uwanja wa Nyayo.

Wasanii wa humu nchini walitilia maneno yao kuhusu matukio hayo huku wakisema haikuleta picha nzuri kuleta wasanii kutoka nje hali ya kuwa nchini kuna wasanii wazuri tena wenye ufuasi mkubwa.

Wa hivi punde kutilia neno katika mjadala huyo ni mchekeshaji na muigizaji Alex Mathenge ambaye amesema wasanii wengi wa humu nchini wanaogopa kujihusisha na mirengo ya kisiasa hadharani kutokana na kuogopa kupoteza dili zao na makampuni mbalimbali yanayowarambisha madili ya kuwa balozi wa mauzo katika biashara zao.

“Sababu kubwa ni kwa nini wasanii wa Kenya hawakuwa katika hafla ya Azimio na badala yake Diamond Platnumz aliwakilisha ni kwamba sisi ni waathiriwa wa kupoteza biashara. Utatumbuiza pale na kupoteza dili zote za kibiashara kuanzia,” alisema Mathenge.

Wasanii wenzake walionekana kukubaliana naye huku baadhi wakilaumu makampuni ambayo yanawapokonya wasanii ubalozi pindi tu wanapoonesha mapenzi yao kwa mirengo fulani ya kisiasa humu nchini.

“Wakati mwingine washirika wa kibiashara wanapaswa kuelewa kwamba wasanii pia wanafanya biashara inapokuja suala la uidhinishaji, maonyesho na ushawishi. Ikibidi unifungie nje ya biashara fulani, basi ulipe kinachostahili kupuuza biashara zingine. Maoni yangu hayajazuia ukuaji wa mashabiki wangu. , maoni yangu na ushirikiano wa ushirika.Kuwa na namba, jua thamani yako na kamwe hutapiga magoti kwa mtu yeyote.Tunahitaji kuacha siasa za mapepo,” mchekeshaji Victor Naaman aliandika.