"Hakuna kitu zaidi ninachotaka maishani!" Massawe Japanni afichua ombi lake kuu la kila siku

Massawe amebainisha kuwa baraka kubwa zaidi ambayo amewahi kushuhudia maishani ni kuwa mzazi.

Muhtasari

•Massawe amemuomba Mungu kumjalia miaka zaidi na afya njema ili aweze kuwalea watoto wake bila shida yoyote.

•Mtangazaji huyo amedokeza kwamba huwa anafurahia sana kutazama jinsi mabinti zake wanavyohusiana.

Image: INSTAGRAM// MASSAWE JAPANNI

Mtangazaji wa Bustani la Massawe kwenye Radio Jambo amebainisha kuwa baraka kubwa zaidi ambayo amewahi kushuhudia maishani ni kuwa mzazi.

Massawe ni mke wa mwanahabari mashuhuri Tom Japanni na mama wa wasichana watatu warembo sana.

Huku bado akiwa katika hali ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, mtangazaji huyo mahiri amemuomba Mungu kumjalia miaka zaidi na afya njema ili aweze kuwalea watoto wake bila shida yoyote.

"Hakuna kitu zaidi ninachotaka maishani! Ombi langu la kimya la kila siku ni miaka zaidi na afya njema niweze kuwalea hawa! Baraka yangu kubwa ilikuwa kuitwa Mama! Naadhimisha miaka 40 na maua yangu," Massawe alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Malkia huyo wa utangazaji wa Kiswahili pia alidokeza kwamba huwa anafurahia sana kutazama jinsi mabinti zake wanavyohusiana.

"Kuwatazama wakizozana na kupigana, kisha kupenda sana, ni mojawapo ya zawadi zangu kubwa," Alisema.

Massawe ambaye ni mmoja wa watangazaji wa Radio wanaotambulika zaidi nchini ni kipenzi cha wengi kutokana na jinsi anavyosawazisha kazi zake nyingi na familia yake kwa ufanisi mkubwa.

Jumatano iliyopita, Julai 27 aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 40.

Huku akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, Massawe alimshukuru Mola kwa miaka 40 ambayo ameishi na kwa yote aliyotimiza katika kipindi hicho.

"40. Wow! Ni hatua muhimu iliyoje! Naweza kusema tu, Asante Mungu! Kila mwaka umekuwa somo, fursa na wakati mwingine hasara. Muhimu zaidi, kila mwaka umekuwa baraka. Asante kwa kuwa sehemu ya safari yangu," Massawe alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha zake nzuri kadhaa zilizoonyesha wazi  jinsi anavyozidi kung'aa kadri miaka inavyosonga.

"Na sasa, kwa  adventure zaidi inayoitwa maisha," Alisherehekea.

Mtangazaji huyo alisherehekea siku yake ya barani Ulaya ambako anaendelea kufurahia likizo ya siku kadhaa.

Sote katika Radio Jambo tunamtakia Massawe Japanni maisha marefu!