Muigizaji Onyi azungumzia maendeleo yake baada ya kupelekwa Rehab

Muhtasari

• Onyi amesema tayari ameshuhudia mabadiliko na kueleza kuwa anafurahia safari ya kupambana na uraibu wake.

•Amesema baada ya kukamilisha kipindi cha marekebisho anakusudia kutembelea shule mbalimbali na vituo vingine mbalimbali akitoa mawaidha kwa watu.

Mwigizaji William Okore almaarufu Onyi
Mwigizaji William Okore almaarufu Onyi
Image: SCREEN GRAB// TUKO EXTRA

Muigizaji William Okore almaarufu 'Onyi' kutokana na kipindi cha Real Househelps of Kawangware anaendelea kupambana na uraibu wake wa pombe baada ya kujiunga na kituo cha marekebisho (Rehab) takriban mwezi mmoja uliopita.

Akizungumza na Tuko, Onyi alisema tayari ameshuhudia mabadiliko na kueleza kuwa anafurahia safari ya kupambana na uraibu wake.

"Ni kitu poa. Nimeona mabadiliko. Nikiingia mikono yangu ilikuwa inatetemeka. Mabadiliko ni makubwa sana. Niko karibu kumaliza mwezi mmoja na nimefurahia  kitu moja, watu wanasema nimekuwa mweupe," Onyi alisema.

Muigizaji huyo amedai kuwa  ameweza kujifunza mengi katika kipindi ambacho amekuwa pale na ameanza kurejelea maisha ya kawaida.

Onyi amesema baada ya kukamilisha kipindi cha marekebisho anakusudia kutembelea shule na vituo vingine mbalimbali akitoa mawaidha kwa watu.

"Kuna watu wengi ambao wanapitia shida kama hii. Ata mimi naweza kupitia kwa mashule na kazi za watu nikiwashauri. Kuna watu wako kwa kazi nzuri sana, hatuwezi taka kupoteza watu kama wale," Alisema.

Mwezi Machi muigizaji huyo alikiri wakati janga la Corona lilikumba dunia alijipata akipiga maji kila siku ili aweze kupata usingizi.

"Mimi hukunywa, nisteam ili nipate usingizi kwa sababu sifikirii. Sina nafasi na wakati wa kufikiria. Nikikutana na mtu kwa njia, ananitoanisha eti sina kitu. Ata ombaomba nikikutana naye mjini ananiuliza kwani kazi kuliendaje.. wacha nikate maji kidogo ili nipate usingizi kwa sababu nikiingia kwa nyumba, mtu amenitukana vibaya nami nimeichukulia tu kwa roho," Onyi alisema katika mahojiano.

Onyi alikejeliwa sana baada ya kujitokeza na kusimulia masaibu yaliyomkumba baada ya kupoteza kazi zake za  usanii.