"Nilishtuka!" Karen Nyamu afichua uhusiano wake na Mustapha huku akitoa msaada wake

Alifichua kwamba tayari ametuma wawakilishi wake kumtembelea mamake Mustapha na kutoa msaada wake.

Muhtasari

•Nyamu alifichua kuwa yeye na Mustapha walikuwa marafiki na akakiri kushtushwa na matukio ya hivi majuzi.

•Nyamu alitoa wito kwa mashabiki wa msanii huyo kuingilia kati na kutoa mchango wa kumsaidia kutoka katika hali aliyozama.

amesema amewatuma wawakilishi wake kumtembelea mamake Mustafa ambaye anaugua saratani.
Karen Nyamu amesema amewatuma wawakilishi wake kumtembelea mamake Mustafa ambaye anaugua saratani.
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amebainisha kuwa alishtuka sana baada ya kupata taarifa kuhusu hatma ya mwanamuziki mkongwe wa Kenya Daud Mustapha almaarufu Colonel Mustafa ambaye amekuwa akiteseka kimyakimya.

Masaibu yaliyompata mtumbuizaji huyo aliyeshabikiwa sana katika miaka ya nyuma yalipata kudhihirika wiki jana baada ya video yake akifanya kazi katika eneo la ujenzi kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. Baadaye, alikiri kwamba amekuwa akifanya kazi za kawaida ili kumudu maisha na kumhudumia mama yake anayepambana na saratani baada ya taaluma yake ya muziki kufeli miaka michache iliyopita.

Akizungumzia suala hilo, Nyamu alifichua kuwa yeye na Mustapha walikuwa marafiki na akakiri kushtushwa na matukio ya hivi majuzi.

"Mustapha ni rafiki yangu wa zamani na kumuona akiwa katika hali hiyo kumenishtua pia," Nyamu alisema siku ya Jumatatu.

Mwanasiasa huyo wa chama cha UDA aliendelea kufichua kwamba tayari ametuma wawakilishi wake kumtembelea mama yake Mustapha na kutoa msaada wake kwa familia ya nguli huyo wa muziki.

Aidha, alitoa wito kwa mashabiki wa msanii huyo kuingilia kati na kutoa mchango wa kumsaidia kutoka katika hali aliyozama.

"Huku nikiwa nimesafiri, timu yangu ilimtembelea mamake Mustapha ambaye ni mgonjwa na kutoa msaada wangu binafsi.

Huu ni wito kwa mashabiki wake ambao wako tayari kusaidia familia kwa njia ndogo unayoweza na mbarikiwe," aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook na kuambatanisha ujumbe huo na picha ya bango la ombi la msaada kwa ajili ya gharama ya matibabu ya mamake Mustapha.

Image: HISANI

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Eve Mungai, Mustapha alitaja kuwa anahitaji kazi au mtaji kuanzisha biashara ili aweze kuweka chakula mezani na kulipa bili kadhaa. Alibainisha kuwa shida yake kubwa kwa sasa ni matibabu ya gharama kubwa ya mama yake kwani anaugua ugonjwa wa saratani.

“Sifikirii kufanya muziki; Nahitaji kazi, kitu ninachoweza kufanya, ili kujisaidia. Ninaweza kusimamia klabu, naweza kufungua duka na pia nina duka ambalo liko karibu kufungwa kwa sababu ‘nimekula hisa yote,” alisema.

Alikiri kuwa kazi yake ya muziki imekuwa haifanyi vizuri na kila anapotoa wimbo hauvumii na kuongeza kuwa huwa hapati mapato kutokana na nyimbo zake za awali.

"Mziki haijakuwa ikifanya vizui, kila nikitoa muziki inakataa."alisema.

Kulingana na Mustapha, dhiki zake zilianza 2020, wakati wa Corona.