Pasta Kanyari apewa mafunzo ya ushauri, aombewa kufuatia matukio ya kutatanisha mitandaoni

Dkt Mutua pia alichukua muda kumwombea pasta huyo huku akiwa amepiga magoti mbele yake.

Muhtasari

•Mkutano huo uliofanyika katika eneo lisilofichuliwa siku ya Ijumaa unafuatia matukio ya hivi majuzi ya kutatanisha ya pasta huyo.

•Kanyari aliomba msamaha kwa Wakenya baada ya kupokea zawadi ikiwa ni pamoja na pakiti ya kondomu kwenye madhabahu ya kanisa lake.

alikutana na pasta Kanyari Ijumaa
Ezekiel Mutua alikutana na pasta Kanyari Ijumaa
Image: X// Dr. Ezekiel Mutua

Mchungaji wa Kenya aliyezingirwa na utata mwingi, Victor Kanyari ameshiriki kikao maalum na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uainishaji wa Filamu nchini (KFCB), Dkt. Ezekiel Mutua.

Mkutano huo uliofanyika katika eneo lisilofichuliwa siku ya Ijumaa unafuatia matukio ya hivi majuzi ya kutatanisha ya pasta huyo kwenye mitandao ya kijamii ambayo yameibua shutuma nyingi.

Katika taarifa kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, Dkt Mutua alifichua kuwa pasta Kanyari alianza kupokea mafunzo ya ushauri kufuatia matendo yake.

“Nipo hapa na Mchungaji Kanyari. Tumeanza mafunzo ya ushauri. Mnataka nimwambie aje?” Ezekiel Mutua aliandika siku ya Ijumaa mchana.

Aliambatanisha taarifa yake na picha yake na Kanyari wakiwa wamekaa pamoja kwenye meza katika eneo lisilofichuliwa.

Mkutano huo unakuja katika wakati ambapo pasta huyo mwenye utata amekuwa akipokea shutuma nyingi kutoka kwa wanamtandao kufuatia matendo yake ya hivi majuzi.

Bosi huyo wa MCSK pia alichukua muda kumwombea pasta huyo huku akiwa amepiga magoti mbele yake.

Siku ya Alhamisi, aliomba msamaha kwa Wakenya baada ya kupokea zawadi ikiwa ni pamoja na pakiti ya kondomu kwenye madhabahu ya kanisa lake.

Katika video ambayo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Kanyari alisimulia kilichotokea.

"Msichana kutoka ukambani aliniletea kondomu katika madhabahu. Sikujua, mimi nimefanyia Mungu kazi kwa miaka 30 na sijawahi ona mtu ambaye anaweza leta vitu kama hizo katika madhabahu."

Aliongeza "Hakuna mtu hakoseangi, msichana huyo alikosea na mimi pia sikutaka kumpiga maana ningeongea angepigwa na washirika."

Alisema kuwa mwanadada huyo alikuwa mwanatiktok ambaye alimuona mhubiri huyo kwenye mtandao huo wa kijamii na kuamua kutembelea kanisa lake. Aliongeza kuwa bibi huyo hajaokoka.

"Nimekuja kuomba msamaha. Naomba mnisamehe kwa jambo hilo. Na jambo kama hilo halitajirudia tena."

Kanyari alisema alifungua zawadi hizo akidhani ni kwa ajili ya 'kupanda mbegu' ndipo alipopatwa na mshtuko.

Hapo awali, Dkt Ezekiel Mutua alikuwa amejitokeza akizungumzia kuhusu kasisi huyo akidai kuwa angetoa taarifa ambayo ingemfanya apigwe marufuku kutoka kwa TikTok na afungwe jela.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa MCSK alidai kuwa Kanyari anadaiwa kudhalilisha jina la pasta na pia makasisi wote.