'Siwezi kuishi bila wewe, ulikuwa wakati mbaya zaidi maishani!' Mwajiri wa Rosie akiri akimkaribisha tena

Bi Roseline Atieno almaarufu Nanny Rosie aliungana tena na mwajiri wake wa Lebanon siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Rosie aliwakumbatia watoto hao, akawainua juu na hawakutaka kushuka mikononi mwake hata wazazi wao walipojaribu kuwachukua.

•Mwajiri huyo wa Lebanon alikiri kwamba alishukuru sana kuona Rosie akirudi kwao licha ya kupewa kazi zingine nyingi.

Image: HISANI// MARIA CATALEYA

Ilikuwa wakati wa hisia sana huku mwanamke wa Kenya aliyevuma sana mitandaoni mwezi uliopita, Bi Roseline Atieno almaarufu Nanny Rosie akiungana tena na mwajiri wake wa Lebanon siku ya Jumatatu.

Rosie ambaye alipata umaarufu mwishoni mwa mwaka jana kufuatia video yenye hisia kali ya yeye akiiga familia ya mwajiri wake alirejea Lebanon siku ya Jumatatu baada ya kuwa na familia yake nchini Kenya kwa karibu miezi miwili. Waajiri wake na watoto wao wawili wadogo walimkaribisha kwenye uwanja wa ndege ambapo walikuwa na muungano mzuri sana.

Mama wa watoto hao wawili ambao Rosie amekuwa akiwalea kwa takriban miaka miwili iliyopita alizidiwa na hisia baada ya kumuona na alitumia nafasi hiyo kukiri jinsi maisha yalivyokuwa magumu bila yeye kuwepo.

“Karibu tena Rosie. Siwezi kuishi bila wewe kwa kweli. Ilikuwa wakati mbaya zaidi maishani mwangu," mwajiri wa Rosie alimwambia kwenye video ambayo alishiriki kwenye mtandao wa kijamii.

Watoto hao wawili warembo wanaoonekana kuwa na uhusiano mzuri sana na mwanadada huyo kutoka Bondo, Kaunti ya Siaya walifurahi sana kumuona amerudi na hawakuweza kuficha furaha yao huku wazazi wao wakirekodi tukio hilo la kuungana tena lenye hisia.

Katika video hizo, Rosie aliwakumbatia sana watoto hao, akawainua juu na hawakutaka kushuka mikononi mwake hata wazazi wao walipojaribu kuwachukua.

"Inaonekana watakaa na Rosie, Mama atasafiri," mwajiri huyo anayejitambulisha kama Maria Cataleya kwenye mtandao wa kijamii alisema.

Mwajiri huyo wa Lebanon alikiri kwamba alishukuru sana kuona Rosie akirudi kwao licha ya kupewa kazi zingine nyingi.

"Rosie alitimiza ahadi yake na kurudi kwa mapacha ingawa alipata ofa nyingi. Upendo wa kweli utashinda kila wakati," alisema.

Katika mahojiano ya Desemba mwaka jana baada ya kurejea Kenya, Rosie alisema alijisikia vibaya sana kuwaacha wanandoa ambao amewafanyia kazi tangu Oktoba 2021 pamoja na watoto wao wanne ambao alikuwa akiwatunza.

"Ilikuwa wakati wa huzuni zaidi maishani mwangu. Ilijawa na hisia tofauti kwa sababu kwa upande mmoja nilifurahi kuja kukutana na familia yangu na kwa upande mwingine nilikuwa na huzuni kwa sababu nilikuwa naacha watoto ambao nimeishi nao kwa miaka miwili,” Rozzie alisema.

Mwanamke huyo anayetoka Bondo katika Kaunti ya Siaya pia alifunguka kuhusu uhusiano mzuri na muungano thabiti kati yake na watoto wa mwajiri wake.

Alisema alijisikia kukaribishwa sana alipokuwa na familia ya Lebanon kwani wote walimtendea vyema na walithamini kazi nzuri aliyowafanyia.

“Hapo nilijisikia kuwa nyumbani. Tofauti pekee ni mimi nilikuwa nalipwa. Ninawapenda watoto kwa sababu wanathamini kazi yangu na wananipenda kwa hilo. Walikuwa wakinichukulia kama mzazi wao,” alisema.