"Tunakumiss sana" Anerlisa amkumbuka kwa hisia marehemu dada yake, Tecra Muigai

Tecra aliaga dunia mnamo Mei 2, 2020 baada ya kuanguka kwenye ngazi za hoteli ya Lamu.

Muhtasari

•Anerlisa Muigai ameadhimisha mwaka wa tatu wa kifo cha marehemu dada yake mdogo, Tecra Wangari Muigai.

•Anerlisa alimhakikishia marehemu dadake kuwa kumbukumbu zake bado ziko mioyoni mwao miaka mitatu baadaye

amemkumbuka marehemu dada yake, Tecra Muigai
Anerlisa Muigai amemkumbuka marehemu dada yake, Tecra Muigai
Image: INSTAGRAM// ANERLISA MUIGAI

Mfanyibiashara Anerlisa Muigai ameadhimisha mwaka wa tatu wa kifo cha marehemu dada yake mdogo, Tecra Wangari Muigai.

Tecla aliaga dunia mnamo Mei 2, 2020 baada ya kuanguka kwenye ngazi za hoteli ya Jaha House, katika eneo la Shela, kaunti ya Lamu.

Huku akimkumbuka mdogo huyo wake siku ya Jumanne, Anerlisa alikiri kwamba yeye na familia nzima wanamkosa sana maishani.

"Leo, ninakuheshimu na kusherehekea upendo, furaha, na nuru ambayo ulileta katika maisha yetu. Tunakukumbuka sana, lakini tunapata faraja kwa kujua kwamba uko mahali pazuri zaidi unatuangalia," alisema katika taarifa.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa kampuni ya maji ya Nero Limited alimhakikishia marehemu dada yake kuwa kumbukumbu zake bado ziko mioyoni mwao miaka mitatu baada ya kuaga dunia kufuatia tukio la kutisha sana.

"Ingawa hauko nasi tena kimwili, roho yako inaendelea kuishi, na urithi wako daima hunitia moyo. Tecki hukuwa dada tu, bali pia rafiki, msiri, na chanzo cha nguvu. Ulileta furaha, kicheko, na uchangamfu kwa familia yetu," alisema.

Anerlisa Muigai aliambatanisha ujumbe huo wa kihisia na picha ya kumbukumbu akiwa pamoja  na mdogo huyo wake.

Marehemu Tecra Muigai alikuwa mtoto wa nne na wa mwisho wa mmiliki wa Keroche Breweries Tabitha Karanja.

Anerlisa alikuwa na uhusiano wa karibu mno na marehemu dada yake na mara nyingi amekuwa akionyesha wazi kuwa kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwake na bado hajaweza kukabiliana na hali ile kabisa.

Kitendawili kuhusu kifo cha Tecra bado hakijatatuliwa na miaka mitatu baadaye bado kuna kesi inayoendelea mahakamani.

Mridhi huyo wa Keroche alikuwa na mpenzi wake Omar Lali wakati alipoanguka na kuugua majeraha yaliyopelekea kifo chake. Matokeo ya uchunguzi wa maiti yalionyesha kuwa inawezekana marehemu alipigwa na kitu butu kichwani na kusababisha majeraha ambayo yalisababisha kifo chake.

Kulingana na matokeo yaliyowasilishwa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor, Tecra, wakati huo akiwa na umri wa miaka 29, alikuwa amevunjika fuvu la kichwa na kuvuja damu ndani ya ubongo. Ubongo ulikuwa umevimba.