DPP aigeuzia joto afisi ya Ruto, kuhusu barua "feki"

ITUMBI.1.jfif
ITUMBI.1.jfif
Katibu wa dijitali na mawasiliano Dennis Itumbi anafikishwa mahakamani leo Alhamisi kufuatia kukamatwa kwake siku ya Jumatano na maafisa wa ujasusi.

Itumbi alikesha katika kituo cha polisi cha Muthaiga alikopelekwa baada ya kuhojiwa katika makao makuu ya DCI kuhusiana na barua “feki” iliyodai kuwepo kwa njama ya kumuua naibu rais William Ruto.

Wakili wake Moses Chelang’a alisema walikuwa bado hawajaelezwa tuhuma dhidi ya mteja wake.

Maafisa wa upelelezi wamegeuzia joto afisi ya naibu rais William Ruto kuhusiana na barua iliyodai kwamba kundi moja la mawaziri na maafisa wakuu wa idara za serikali walikutana kupanga njama ya kumwangamiza Ruto.

Itumbi ambaye ni mwandani wake Ruto alikamatwa katika barabara ya Mama Ngina mjini Nairobi na kuzuiliwa katika korokoro ya polisi ya Muthaiga huku mkurugenzi wa DCI George Kinoti akiimarisha juhudi za kubaini chanzo cha madai ya kuwepo kwa najama ya kumwangamiza naibu rais.

Hatua hii huenda ikazidisha uhasama katika serikali. Wandani wa Ruto wanamshtumu DCI kwa mapendeleo na kutafuta njia kusambaratisha uchunguzi kuhusu madai ya kupanga njama ya kumuua Ruto.

Itumbi alihudumu kama mkurugenzi wa dijitali katika Ikulu ya Rais licha ya utata kuhusu kisomo chake.

Maafisa wa ujaisusi wanaamini kuwa Itumbi ndiye aliyeandika barua hiyo feki ya Mei 30 ambayo ilidai kuwepo kwa mkutano katika Hoteli ya La Mada kujadili vile ya kuimarisha juhudi za kumuunga mkono rais Kenyatta katika eneo la kati na katika maeneo mengine.

Pia katika agenda ya mkutano huo baraua hiyo inadai kujadiliwa kwa pendekezo la kufanyika kwa kura ya maamuzi na kuanzisha mikakati ya kumkabili Ruto.