DPP apinga Sonko kuachiliwa, adai ana historia ya kutoroka gerezani

mike Sonko
mike Sonko
Ofisi ya mkurugenzi wa mwendesha mashtaka ya umma DPP imepuulizia mbali ombi la gavana wa Nairobi Mike Sonko kuachiliwa kwa dhamana.

Sonko pamoja na maafisa wengine wa kaunti ya Nairobi waliwasilishwa mbele ya hakimu anayeshughulika na kesi za ufisadi Douglas Ogoti katika mahakama ya Milimani.

Sonko anakabiliwa na makosa ya ubadhirifu wa shilingi milioni 357 katika City Hall.

Mwendesha mashtaka alinukuu kisa ambacho mnamo Machi 12, 1998, Sonko alishtakiwa kwa kukosa kujiwasilisha kortini Mombasa jinsi ilivyotakikana.

Aidha, alishtakiwa na kupigwa faini ya shilingi 500,000 katika kesi ya kwanza na 200,000 kwa kesi ya pili.

Na alitakiwa kuhudumu kifungo cha miezi sita gerezani kwa kila kesi iwapo angeshindwa.

Mwendesga mashtaka Gitonga Riungu na Kihara James ambayo waliwasilisha afisi ya DPP, walikataa kumwachilia kwa dhamana huku wakidai aliwaitoroka gerezani awali.

Kihara alimnukuu kamishina wa gereza ambaye alisema kuwa Sonko alikuwa kizuizini  Shimo La Tewa na alikuwa ameendea matibabu katika Coast General Hospital ambapo alitoroka.

Alitiwa mbaroni baadaye aliposakwa na maafisa wa polisi.

Kihara kupitia hati kortini alisema kuwa kuna kesi nyingine Mombasa ya 2001 inayomkabili Sonko.

Kulingana na Kihara, Sonko anawezakosa kujiwasilisha kortini iwapo ataachiliwa kwa dhamana.

Aidha alisema kuwa kuachiliwa kwake kutaathiri ushahidi kwa kuwa Sonko amekuwa akiwatishia wachunguzi wa EACC dhidi ya kesi inayomkabili.

Kihara alirai jaji kuwaamuru washtakiwa wa kesi za ufisadi kuwasilisha paspoti zao ili wasitorokee ughaibuni.