Mmoja afariki katika makabiliano baina ya Polisi na Al shabaab

Afisa mmoja wa polisi wa akiba aliuawa na mwenzake kujeruhiwa katika makabiliano makali baina ya vikosi vya usalama na wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab usiku wa Jumatatu. Kisa hicho kilitokea katika eneo la Dawaduba, Fino Kaunti ya Mandera.

Polisi walisema mwanamgambo mmoja wa Al shabaab pia aliuawa wakati wa oparesheni hiyo ya pamoja ya vikosi vya usalama.

Oparesheni hiyo ilikuwa ya kuwafurusha wanamgambo wa kundi hilo kutoka himaya ya Kenya.

Wapiganaji hao walikuwa wamepiga kambi katika ardhi ya Kenya wakati vikosi vya usalama vilipopashwa habari na kuvamia eneo hilo.

Makabiliano makali yaliendelea kwa saa kadhaa na kunahofu kuwa huenda kuna idadi kubwa ya wahasiriwa.

Idara ya usalama imesema kwamba oparesheni hiyo bado inaendelea.

Mwezi uliyopita wanamgambo wa Al Shabaab walivamia kijiji cha Hereri karibu na mji wa Mandera na kuiba chakula.