Jose Mourinho ateuliwa meneja mpya wa Spurs

Jose Mourinho ameteuliwa rasmi kuwa meneja mpya wa Tottenham Hotspurs kuchukuwa nafasi ya Mauricio Pochettino aliyepigwa kalamu siku ya Jumanne.

Mourinho ambaye aliwahi kuvifunza vilabu vya Chelsea na Manchester United ametia saini mkataba wa hadi mwaka 2023.

"Ubora wa kikosi na chuo cha wachezaji chipukizi vinanifurahisha," Mreno huyo mwenye umri wa miaka 56 alisema. " Kufanya kazi na wachezaji hawa ndilo jambo lililonivutia."

Mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy alisema: "Katika Jose tuko na moja wapo wa maneja bora zaidi katika soka."

Mourinho amekuwa bila klabu tangu alipofutwa na Manchester United Disemba mwaka 2018.

Anachukuwa wadhifa huu wakati spurs wakishikilia nafasi ya 14 katika jadwali la ligi ya primia bila ushindi katika mechi tano zilizopita.

Pochetino ambaye ni raia wa Argentina aliongoza vijana hao wa London Kaskazini kufika fainali ya dimba la ligi ya mabingwa barani Ulaya walikolazwa na Liverpool.