Je, Uhuru na Raila wanamnoa Matiang'i kwa wadhifa wa urais, 2022?

matiang'i uhuru
matiang'i uhuru
Waziri mwenye ushawishi mkubwa serikalini Fred Matiang’i anaripotiwa kupanga kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais baada ya ripoti kwamba amepokea uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wakuu wawili wa kisiasa nchini.

Madai haya yaliibuka baada ya Matiang’i na naibu rais William Ruto kutofautiana hadharani – ishara ya uhasana baina ya wawili hao – ambao huenda wakakutana katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022.

Katika mrengo wa Ruto kuna hofu kwamba Matiang’i anatayarishwa na watu mashuhuri, wakiwemo watu wenye ushawihshi katika familia ya rais. Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga wanasemekana kumuandaa kisiri Matiang’i kama mngombea urais wa maafikiano.

Matiang’i siku za hivi majuzi amefanya ziara nyingi sana katika ngome ya Raila akiandamana na viongozi kadhaa wa ODM, akizindua miradi ya maendeleo na kuongoza mikutano ya harambee.

Waziri huyo jasiri amekuwa pia akizindua miradi mingi katika maeneo ya Kisii, kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono kutoka eneo analotoka.

Huenda akajaza pengo aliloacha aliyekuwa waziri Simion Nyachae aliyestaafu miaka 12 iliyopita kama msemaji wa jamii ya Abagusii.

Tangu “handshake”, waziri huyo anamheshimu sana Raila na amenukuliwa katika mikutano mingi sana ya umma akimlimbikizia sifa Raila, kama kiongozi wa kitaifa.

Ishara dhahiri kuhusu ushawishi wa Matiangi ilikuwa siku ya Ijumaa katika kaunti ya Kirinyaga, alipoongoza viongozi kadhaa wanaounga mkono ushirikiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wakiwemo magavana sita na takriban wabunge 50 kuchangisha pesa.

Matiang’i ni mwenyekiti wa kamati kuu ya mawaziri inayosimamia utekelezwaji wa miradi ya maendeleo kote nchini. Cheo hiki kilionekana kumpunguzia mamlaka naibu rais William Ruto ambaye alikuwa akizunguka kila pembe ya nchi akizindua miradi ya maendeleo.

Siku moja kabla ya kuongoza harambee ya Kirinyaga, Matiang’i alikuwa ametumwa na rais Uhuru Kenyatta kuongoza mnada wa mbuzi katika kaunti ya Kajiado ambapo aliandamana na waziri wa mazingira Keriako Tobiko na gavana Joseph Ole Lenku.

Wakati wa hafla ya Kirinyaga, matiang’i hadharani alimkashifu naibu rais William Ruto na kuwatetea rais Kenyatta na kinara wa Upinzani Raila Odinga huku akipingia dembe BBI.

Mataing’i hadharani alisema kwamba alikuwa ametumwa na rais Uhuru Kenyatta na Raila “ viongozi wetu wawili”.

“Rais Uhuru Kenyatta anafahamu kwamba tuko hapa na ametuma mchango wake, pia mheshimiwa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ametuma mchango wake kupitia naibu kiongozi wa ODM Hassan Joho,” Matiang'i alitangaza.

Ishara kwamba anaungwa mkono na eneo la Kisii, Matiangi aliwasili Kirinyaga akiandamana na karibu viongozi wote waliochaguliwa wa eneo hilo wakiwemo magavana James Ongwae wa Kisii na John Nyangarama wa Nyamira.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Gavana Joho wa Mombasa, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli. Siku ya Jumapili Ruto aliyeonekana kugadhabishwa alimshambulia Matiang’i na kumshtumu kwa kuwa na kiburi na kukosa heshima.

“Nataka kila mtumishi wa umma aliyepewa kazi na rais Uhuru Kenyatta na utawala wa Jubilee kuwacha kujipiga kifua, kuwacha kiburi na kuwacha kukosa heshima,” Ruto alifoka.

Akizungumza katika kaunti ya Kiambu, Ruto alikumbusha mawaziri kwamba waliteuliuwa kwa hisani ya serikali ya Jubilee na kupuuzilia mbali madai ya Matiang’i kuwa walikuwa wakifanya kazi kwa hisani ya rais.